Mwenyekiti wa umoja wa Vyama vikuu vya wakulima wa Tumbaku Tanzania (TCJE) Ndg Emmanuel Cherehani akisisitiza jambo wakati akiwasilisha risala ya wakulima mbele ya Mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) kwenye hafla ya uzinduzi wa msimu wa zao la Tumbaku mwaka 2019 Wilayani Urambo Mkoa wa Tabora, leo Tarehe 13 Mei 2019. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Katikati) akizungumza na Mkurugenzi wa Uzalishaji wa kampuni ya Alliance One Ndg David Mayunga (Kulia) sambamba na Mwenyekiti wa umoja wa Vyama vikuu vya wakulima wa Tumbaku Tanzania (TCJE) Ndg Emmanuel Cherehani mara baada ya mkutano wa wadau wa wa sekta ya Tumbaku katika hafla ya ufunguzi wa msimu wa masoko ya Tumbaku mwaka 2019 iliyofanyika katika maghala ya kampuni ya Alliance One Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, leo Tarehe 13 Mei 2019.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Tabora
Kutoazingatiwa kwa kalenda ya uzalishaji ya zao la tumbaku ni miongoni
mwa ucheleweshaji wa uagizaji wa pembejeo za zao la Tumbaku, Kupungua kwa
mahitaji ya tumbaku na kushuka kwa bei ya tumbaku kwa kila mwaka ni miongoni
mwa mambo yanayowasababishia wakulima hasara.
Hayo yameelezwa leo tarehe 13 Mei 2019 na Mwenyekiti
wa umoja wa Vyama vikuu vya wakulima wa Tumbaku Tanzania (TCJE) Ndg Emmanuel
Cherehani wakati akiwasilisha risala ya wakulima mbele ya Mgeni rasmi ambaye ni
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) kwenye hafla ya uzinduzi wa msimu wa
zao la Tumbaku mwaka 2019 Wilayani Urambo Mkoa wa Tabora.
Cherehani alisema kuwa Makampuni ya ununuzi wa tumbaku
yamekuwa yakipunguza mahitaji yao mwaka hadi mwaka kutoka uzalishaji wa kilo
100,000,000 na kufikia uzalishaji wa mkataba ni kilo 54,000,000 tu katika msimu
wa mwaka 2018/2019 na matarajio ya msimu
ujao wa 2019/2020 ni kilo 43,000,000 baada ya kampuni moja ya ununuzi wa
tumbaku kutoonesha nia ya kuendelea na biashara ya tumbaku nchini.
Alisema, kushuka kwa mahitaji ya wanunuzi kumekuwa kukiendana na
kushuka kwa bei ya wastani ya kuuzia tumbaku mwaka hadi mwaka, ambapo iliwahi
kufikia bei ya wastani wa USD 2.4 lakini mpaka sasa kwa masoko yaliyofunguliwa
wastani ni USD 1.72 na sura iliyopo kwa wanunuzi haioneshi kupanda kwa bei kwa
msimu ujao.
Muwakilishi huyo wa wakulima wa Tumabku nchini aliongeza kuwa
kwa msimu wa 2017/2018 baadhi ya makampuni yameshindwa kulipa ushuru wa vyama
vya msingi na vyama vikuu vya ushirika kwa baadhi ya maeneo kutokana na madai
ya makampuni kutokuwa na uwezo kutokana na madai yao ya muda mrefu ya marejesho
ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT Returns).
Cherehani amemuhakikishia Waziri Hasunga kuwa kwa muda
mrefu wakulima hao wamekuwa na mkakati wa kuanzisha kiwanda cha kusindika
tumbaku ili kuongeza thamani ya zao hilo kwa mkulima na kumuongezea kipato. “Kupitia mradi wa Pamoja wa wakulima wa
tumbaku nchini tumeazimia kuanza upembuzi yakinifu juu ya ujenzi wa kiwanda cha
tumbaku Wilayani Urambo” Alisisitiza
Alisema kuwa kwa kushirikiana na wanunuzi wa zao la
tumbaku vyama vikuu vimeendelea kusimamia utekelezaji wa mipango mbalimbali
ambayo inaendana na vigezo vya uzalishaji wa zao la tumbaku ikiwepo utunzaji wa
mazingira kwa kupanda miti na Uboreshaji wa mabani ya kisasa yenye kutumia kuni
chache ambapo kupitia Vyama vya ushirika kwa msimu wa 2019/2020 kila mkulima
atakuwa ameboresha mabani kwa 100%.
“Pamoja na jitihada za utunzaji wa mazingira, kuna
jitihada zinafanywa za kutafuta nishati mbadala kwa kutumia nishati ya mwanga,
mabingobingo (Elephat grass) na pumba za mpunga kwa maeneo tofauti yanayolima
tumbaku. Tunaomba utafiti huu upewe msukumo mkubwa ili kupunguza matumizi ya
kuni” Alikaririwa Ndg Cherehani
Aidha, wakulima hao wa zao la tumbaku wamempongeza Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Joseph Magufuli,
Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe Kasimu Majaliwa (Mb)
kwa kutetea masilahi ya wakulima kupitia Vyama vya Ushirika.
MWISHO
No comments:
Post a Comment