Sunday, May 12, 2019

WAUGUZI WANAOTUKANA WAGONJWA KUCHUKULIWA HATUA




Na Emmanuel Michael Senny, Kigoma 

WAKURUGENZI wote wa wilaya za mkoa wa Kigoma wametakiwa kuwachukulia hatua wauguzi wazembe na wale wanaotoa lugha chafu kwa wagonjwa ili sekta hiyo iendelee kuheshimika na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa hii leo na Katibu tawala wa mkoa wa Kigoma bw . Rashid Mchatta katika maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani yaliyofanyika kimkoa katika wilaya ya Kibondo  yakiwa na kauli mbiu inayosisitiza kuwa  muuguzi ni mbiu iongozayo afya kwa wote.

 "Muuguzi yeyote yule akibainika akimtukana mgonjwa au akimtolea lugha ambayo si nzuri, achukuliwe hatua stahiki za kinidhamu kama Mtumishi yeyote wa umma na kufuata taratibu za kazi zetu ili sekta ya afya iendelee kuheshimika" alisema Mchatta. 

Aidha aliwataka wananchi kutumia masunduku ya kutolea maoni ama kwenda moja kwa moja kwa uongozi wa hospitali na vituo vya afya iwapo atafanyiwa vitendo visivyo stahili wakati wa kuhudumiwa ili kukomesha watumishi wachache wanaotukana wagonjwa ama kutoa huduma mbovu.

Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma dr. Paul Chawote alikili kuwa mawasiliano kati ya wauguzi na wagonjwa hayaendi vizuri hivyo uongozi unaendelea kulifanyia kazi ili kuondoa kero na lugha mbaya katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

"Mara nyingi kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wagonjwa kuhusu huduma mbovu za wauguzi lakini uongozi umekuwa ukiyashughulikia kwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa wauguzi hao ili kupambana na vitendo vinavyofanywa na wauguzi wasio waadilifu kazini" alisema Chaote.

Mwisho

No comments:

Post a Comment