Na Lorietha Laurence-WHUSM, ARUSHA
Makatibu
Wakuu wa Wizara ya Habari ,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi na
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu , Sayansi na
Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo pamoja na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha
Dkt. Masudi Senzia wamekutana na Viongozi wa Wazee wa Kimasai ili kupata suluhu
la eneo la kimila maarufu kama Oreteti
Loongaik lililopo ndani ya chuo hicho.
Kikao
hicho kimefanyika leo Jijini arusha
katika Ofisi za Kaimu Mkuu wa
Chuo Cha Ufundi Arusha agenda kuu zikiwa
ni kuongezewa eneo ili wazee wa kimila waweze kufanya shughuli zao za mila kwa
nafasi, kupewa kibali cha kujenga nyumba kwa ajili ya kujihifadhi wakati wa
mvua pamoja na kuwa na geti la kuingilia tofauti na geti la chuo.
Makatibu
Wakuu hao walipata wasaa wa kuwasikiliza , kujadiliana pamoja na kutembelea
eneo hilo la kimila ili kuweza kuona ni kwa namna gani wanaweza kutoa maamuzi
ambayo hayataadhiri upande wowote na hivyo kufikia muafaka mzuri.
“Serikali inatambua umuhimu wa kuenzi na
kudumisha mila na ndio maana tupo hapa leo ili kuweza kupata suluhisho la
kudumu kuhusu eneo hili ambalo limekuwapo tangu enzi na enzi” alisema Bibi.
Susan Mlawi.
Aidha
Katibu Mkuu , Bibi. Susan Mlawi aliupongeza uongozi wa chuo kwa kuwaruhusu
Wazee hao kuweza kufanya shughuli za
kimila katika eneo hilo na hivyo kusaidia katika kuendeleza utamaduni.
Naye
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo
aliwataka Wazee hao wa kimila kuendelea kufuata taratibu za kupata kibali
kutoka kwa uongozi wa chuo ili kuweza kufanya vikao vyao vya kimila hadi pale
suluhisho la kudumu litakapofikiwa.
“Mapendekezo
yenu ni mazuri nasi tumeyapokea na tunaahidi kuyafanyia kazi ambapo baada
ya mwezi mmoja tutarudi tena
mahali hapa tukiwa na majibu kutoka kwa viongozi wetu ambao ni Mawaziri wenye
dhamana na Wizara hizi mbili” alisema Katibu Mkuu Dkt. Akwilapo.
Kwa
Upande wa Mwenyekiti wa Wazee wa Kimasai Bw. Laiza Ole Kisongo ameishukuru
Serikali kwa kuona umuhimu wa suala hilo na kuwapa nafasi ya kuweza kujadiliana
kwa pamoja ili kufikia muafaka na kujenga taifa lenye umoja na amani.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment