Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika mkutano wa dharura wa
baadhi ya wadau wa zao la pamba aliouiitisha kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini
Mwanza, Mei 29, 2019. Katikati ni Naibu Waziri wa Viwanda na
Biashara, Mhandisi Stella Manyanya na kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Omari
Mgumba.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa dharura wa baadhi ya wadau wa zao la
pamba wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa wakati alipozungumza katika
mkutano aliouitisha kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Mei 29,
2019.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa dharura wa baadhi ya wadau wa zao la
pamba wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa wakati alipozungumza katika
mkutano aliouitisha kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Mei 29,
2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika mkutano wa dharura
wa baadhi ya wadau wa zao la pamba aliouiitisha kwenye Ukumbi wa Benki Kuu
jijini Mwanza, Mei 29, 2019. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela
na kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa
Wilaya na Wakurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya zinazolima
zao la pamba katika mkutano wa dharura wa baadhi ya wadau wa zao la pamba
kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Mei 29, 2019.
*Amwagiza Katibu
Mkuu Kilimo atume timu ichunguze Bodi ya Pamba
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
ana imani kuwa ununuzi wa zao la pamba utaanza mara moja kwa bei ya sh. 1,200
kwa kilo moja katika mikoa yote inayozalisha zao hilo.
Amefikia uamuzi huo baada ya kuwepo
kwa sintofahamu ya bei kwa takriban ya wiki nne tangu bei elekezi ilipotangazwa
Aprili 30, 2019 mkoani Shinyanga kwamba bei hiyo ianze kutumika kuanzia Mei 2,
2019.
Alikuwa akizungumza na wadau wa sekta
ndogo ya pamba kwenye kikao kilichofanyika leo (Jumatano, Mei 29, 2019) kwenye
ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu, jijini Mwanza. Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu
Mawaziri wa Kilimo na Viwanda, Makatibu Wakuu wa Kilimo na Ofisi ya Rais –
TAMISEMI na Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu na
Geita.
Wengine ni wawakilishi wa Wabunge wa
mikoa hiyo, Makatibu Tawala wa mikoa, Wakuu wa Wilaya zote za mikoa hiyo, na
Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya hizo. Pia kilihudhuriwa na wanunuzi wa
pamba, wakulima na maafisa wa benki kadhaa.
Waziri Mkuu aliwaeleza wajumbe wa
mkutano huo kwamba Serikali bado inaendelea kutafuta njia nzuri ya
kuwakutanisha wadau wa mazao ya kibiashara ili yaweze kuwa na tija kwa
wakulima. Alisema kazi hiyo inafanywa wa Wizara ya Kilimo. Mazao hayo ni pamba,
chai, kahawa, korosho, tumbaku na chikichi.
Pia alisema Bodi ya Pamba iachiwe
jukumu la kutoa leseni za ununuzi wa zao hilo na kwamba Wakurugenzi wa
Halmashauri waliokuwa wakifanya kazi hiyo waache mara moja. “Kuna baadhi ya
Wakurugenzi wanatoa leseni za ununuzi, lakini wenye Mamlaka ni Bodi ya Pamba.
Mnunuzi nenda Bodi ukapate leseni yako,” alisema Waziri Mkuu.
Alitumia fursa hiyo kuwakemea baadhi
ya wakurugenzi ambao wamekuwa wakizuia wanunuzi wapya kwenye maeneo na
kuendelea kuwakumbatia wanaowataka wao. “Wakurugenzi baadhi yenu mnazuia
wanunuzi wapya, mnamtaka fulani tu. Kwa kufanya hivyo, unapungua kiwango cha
kilo ambacho wakulima wako wangeuza,” alionya.
‘Wanunuzi nendeni mkajitambulishe kwa
Wakuu wa Wilaya au Wakurugenzi ili watambue kwamba mpo kwenye maeneo yao lakini
kila mnunuzi anayo haki ya kwenda kununua pamba mahali popote hapa nchini.”
Kuhusu ubora wa pamba, Waziri Mkuu
alitaka wananchi waelimishwe ili waache kuweka maji au mchanga kwenye pamba kwa
minajili ya kuongeza uzito kwani kwa kufanya hivyo wanachafua jina la Tanzania
pindi inapopelekwa kuuzwa nje ya nchi.
Pia alitaka vyama vikuu vya ushirika
vijiridhishe kuhusu ubora wa maghala ya kuhifadhia pamba kwenye vyama vya
msingi (AMCOS) kwani kwa kufanya hivyo, itawasaidia wakulima wauze mapema pamba
yao mara baada ya kuivuna.
Kuhusu mizani, Waziri Mkuu aliiagiza
wakala wa vipimo nchini (WMA) waende wakakague mizani ya kwenye AMCOS na kwenye
vinu vya kuchambulia pamba (ginneries) kwa sbabu ya tofauti kubwa ya uzito
inayojitokeza na kuwalazimisha wakulima kulipia upotevu wa kilo hizo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe atume
wakaguzi kwenye Bodi ya Pamba ili wabainishe matumizi ya sh.100 kwa kila kilo
ambazo zimekuwa zikilipwa kwenye bodi hiyo.
“Katibu Mkuu Kilimo lete wakaguzi
ndani ya bodi ya pamba, waangalie kwa kipindi cha miaka mitatu toka tulipoanza
kukusanya sh. 100 kwa kilo, zimekusanywa shilingi ngapi, na zimetumika kulipia
nini.
“Na Mrajisi wa Ushirika nchini ufanye
ukaguzi kwenye vyama vikuu vya Ushirika na AMCOS. Uangalie ziko ngapi na
zinafanya nini. Kuna AMCOS zina hela, je fedha hiyo imetumika kufanya nini ili
kuendeleza zao la pamba. Je zimenunua matrekta au zimelipia posho za vikao,”
alisema.
Naye Mwenyekiti wa
Chama cha Wanunuzi Binafsi wa Pamba (TCA), Bw. Christopher Gachuma ameshukuru
Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa kuhusu utoaji wa leseni kwani yalikuwa ni
kikwazo kikubwa kwa baadhi ya wanunuzi wa zao hilo.
“Suala la utoaji leseni linapaswa
lianze mapema lakini kuna wengine hadi sasa bado hawajapata leseni zao.”
Aliwataka wanunuzi wa pamba waanze kununua pamba ili msimu wa mauzo uanze kwa
kasi.
No comments:
Post a Comment