Afisa Programu kutoka Eastern Africa Grain Council (EAGC) Bw.Junior Ndesanjo akichangia jambo wakati wa mkutano huo.
Mkurugenzi kutoka TOMONI FARMS Bw.Franklin Bagalla (Mkulima) akieleza namna wakulima walivyojipanga katika kuchangia hoja za masuala ya kilimo katika kongamano linalotarajiwa kuanza Februari 13, 2019 Dodoma ili kujadili na kuchambua sera mbalimbali zinazohusu masualaya mifugo, uvuvi na kilimo.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu, Joseph Kiraiya (kushoto) akiteta jambo na Mratibu wa Jukwaa la Uchambuzi wa Sera za Kilimo Profesa, David Nyange mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari wakati wa maandalizi ya kongamano la Tano la Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Jijini Dodoma,Mkutano ulifanyika Februari 12, 2019 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
NA.MWANDISHI WETU
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Kushirikiana na Wadau wa masuala ya Mifugo,
Kilimo na Uvuvi wameandaa Kongamano la Tano la Wadau wa Sekta hizo ili kujadili
matokeo ya tafiti zinazohusu sera za kilimo na maboresho ya sera hizo ili
kujenga mazingira wezeshi kwa wakulima na sekta binafsi.
Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 mnamo
Februari 13, 2019 Jijini Dodoma.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za
Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu, Joseph Kiraiya alipokutana na waandishi wa
habari hii leo, Februari 12, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo.
Kongamano hilo linalenga kuchambua namna sekta ya kilimo inavyoweza kuwa
msingi na chachu ya mageuzi ya viwanda pamoja na kuainisha mapendekezo ya
maeneo ya kisera ambayo yanahitajika kuboreshwa.
Kaulimbiu ya Kongamano hilo kwa mwaka huu 2019 ni “Mchango wa
Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika Kuhamasisha Mageuzi ya Uchumi na
Viwanda Kupitia ASDP-II”
Aidha, Mgeni rasmi wa kongamano hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe.Angellah Kairuki kwa niaba
ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Akielezea kuwa, kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki
kutoka Sekta binafsi, wakulima, wataaluma, wabia wa maendeleo, watafiti na
wadau kutoka sekta ya Umma na kuwataka waandishi wa habari kuendelea
kulitangaza kongamano hilo kwani linaleta chachu kwa kuzingatia mchango wa
wadau katika kuboresha sera za kilimo ili kufikia mageuzi ya viwanda.
“Wito wa Serikali kwa vyombo vya habari ni kuhakikisha mnaendelea
kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuboresha sera mbalimbali zinazohusu masuala
la kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu ambayo
inahimiza juu ya mchango wa sekta hizo katika kuchochea mageuzi ya
viwanda nchini”,alisema Kiraiya.
Naye Mratibu wa Jukwaa la Uchambuzi wa Sera za Kilimo Profesa, David
Nyange alieleza umuhimu wa kongamano hilo ambalo litatoa fursa kwa wadau
kujadili mada nane ikiwemo; Mazao ya Chakula na Lishe, Mazao ya Biashara, Mazao
mapya, bidhaa mbadala na zile zinazoagizwa nje, Mazao ya Mifugo na Samaki
pamoja na Pembejeo na huduma za kilimo
“Kongamano hili limekuja wakati sahihi kwani kati ya vipaumbele vya ukuaji
wa uchumi, kilimo ndiyo msingi wa ukuaji wa viwanda kwani malighafi
zilizotumika viwandani nyingi zinatokana na kilimo, hiyo kongamano hili ni
muhimu kwani linatupa kujadili na kuchambua sera za kilimo na nini kifanyike
kuwa na kilimo kinachokuwa kwa kasi na kuleta mageuzi ya viwanda,”alisisitiza
Prof.Nyange
Kongamano la Tano la Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhusu
uchambuzi wa Sera linaratibiwa na Jukwaa la Watafiti na wachambuzi wa Sera na
Kilimo linalojulikana kama Policy Analysis Group (PAG) ambapo
inajumuisha Taasisi zaidi ya 19 ikiwemo; ANSAF, ESRF, REPOA, USAID/ASPIRES
(MSU), USAID ENGINE (IESC), AGRA, FSDT, AMDT, EAGC, RESAKSS, FAO/MAFAP, SAGCOT,
ACT, DALBERG, TPSF, ILRI NA TAHA.Aidha kundi hilo linashirikiana na Ofisi ya
Waziri Mkuu na Wizara za sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinashirikiana katika
uratibu. kongamano hilo litafanyika Ukumbi wa mikutano wa Hazina Dodoma kuanzia
tarehe 12 hadi 15 Februari, 2019.
=MWISHO=
No comments:
Post a Comment