Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akijibu maswali, Bungeni jijini Dodoma, Februari 7, 2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema zaidi ya sh. bilioni 500 zimelipwa kwa wakulima wa
korosho kati ya sh. bilioni 700 zinazotarajiwa na kwamba malipo hayo bado
yanaendelea kulipwa kwa wakulima wengine waliosalia.
Amesema
tamko la Rais Dkt. John Magufuli la kwamba Serikali itanunua korosho kwa bei ya
sh. 3,300 ni kwa ajili ya korosho za daraja la kwanza na bei ya
korosho za daraja la pili ni asilimia 80 ya zile za daraja la kwanza.
Ametoa
kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Februari 7, 2019) Bungeni jijini Dodoma
katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu
swali la Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka.
Mbunge
huyo alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu malipo kwa wakulima wa korosho
ambao walikuwa wakilipwa sh. 2,600 kwa kilo wakati Rais Dkt. Magufuli
alisema Serikali itanunua kilo moja ya korosho kwa sh. 3,300.
“Malipo
yanaendelea na sehemu kubwa ni kwa wakulima wenye kilo zaidi ya 1,500, Serikali
itanunua korosho zote kama ilivyoelezwa. Taratibu zinazofanyika ni kuhakikisha
anayelipwa ni muhusika. Wananchi endeleeni kuiamini Serikali yenu.”
Waziri
Mkuu amesema ilikuwa ni lazima kwa Serikali ifanye uhakiki kwa wakulima
hususani wale wenye kilo zaidi ya 1,500 ili kujiridhisha kama ni wakulima,
hivyo baada ya kuhakikiwa wakulima wote watalipwa fedha zao.
Amesema
Januari 27, 2019 alitoa maagizo kwa Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya
Mazao Mchanganyiko wahakikishe hadi Februari 15 mwaka huu wawe wamekamilisha
zoezi la uhakiki na kuwalipa wakulima wote wa zao la korosho.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wadau wa zao la korosho kwenye
kikao kilichofanyika mkoani Mtwara, lengo la kikao hicho ilikuwa ni kupata
taarifa juu ya mwenendo mzima wa bidhaa hiyo kwa msimu wa mwaka 2018/2019.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali haijakiuka sheria
kuhusu suala la watumishi kupandishwa mishahara na kwamba ina nia njema ya
kuhakikisha wanalipwa mishahara na posho nzuri.
Ameyasema
hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga aliyedai Serikali
imekiuka sheria ya utumishi kwa kutopandisha mishahara, ambapo Waziri Mkuu
amesema Serikali haikukiuka sheria, bali iliamua kushughulikia suala
hilo kwa kuanza na uhakiki wa watumishi.
Waziri
Mkuu amesema baada ya kufanya uhakiki na kubaini uwepo kwa watumishi hewa
pamoja na waliokuwa wakitumia vyeti vya kugushi, iliwaondoa na sasa Bodi ya
Mishahara na Maslahi ya Watumishi wa Umma inafanya mapitio ya mishahara baada
ya kubaini tofauti, hivyo watumishi waendelee kuwa watulivu.
No comments:
Post a Comment