Kikundi cha Mwiduka kutoka Mkoani Mbeya kikitoa burudani katika tukio hilo la mkutano wa utambulisho kwa vyombo vya Habari, Zanzibar.
NA ANDREW CHALE, ZANZIBAR
WAFANYABIASHARA na wananchi wote wa
Zanzibar, wametakiwa kuwa kifua mbele kila msimu wa uwepo wa tamasha kubwa la
Kimataifa la muziki la Sauti za Busara kwa kuwa tamasha hilo linabeba taswira
chanya ya maendeleo ya Wanzibar wote.
Ambapo pia amewataka kuchangamkia
fursa ya uwepo wake kila mwaka kwani limekuwa likileta wageni
wengi wanaokuja nchini kuhudhuria tukio hilo kubwa lenye kuvutia
watu mbalimbali Duniani kote.
Akizungumza katika mkutano na
Waandishi wa Habari mjini hapa, Mwenyekiti wa Bodi ya Busara Promotions, Simai
Mohammed Said, amesema tamasha hilo la siku nne ni kichocheo cha uchumi kwani
watu wanafika mbali na kulishuhudia lakini pia wanafanya manunuzi na matumizi
ndani ya Visiwa hivyo na kuongeza pato la Serikali.
“Kuanzia leo
tutashudia burudani ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali wa ndani
na nje, wanamuziki hao wataonesha nyimbo za tamaduni za Nchi zao
huku pamoja na kutoa burudani na mafunzo kwa watu wote.
Muziki ni biashara, muziki ni kazi na
ni kazi kubwa hivyo ili kuwaunga mkono wasanii hawa ni kujitokeza kushuhudia
tamasha hili ambapo pia tumetoa ofa ya punguzo kubwa kwa wenyeji.” Alisema
Simai.
Aidha, Simai alisema viongozi wa
Busara Promotions ambao ni waasisi na waandaaji wa tamasha hilo,
wamekuwa wakifanya kila aina ya mbinu kuhakikisha linaandaliwa na kufanyika kwa
ubora uliokusudiwa hivyo ni juu ya wananchi haswa wazanzibar
kulikubali na kulithamini ili kuinua hadhi ya Zanzibar kimataifa.
“Ili tamasha ni la kwenu Wazanzibar.
Tuliinue tulipendemilango ipo wazi kwa wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi
kulidhamini kwa aina yoyote ile ya udhamini utapokelewa. Tunahitaji liweze
kuwa thamani zaidi na tulienzi kwa kiwango cha juu” alisema Simai
ambapo amesisitiza kuwa uwepo wa tamasha hilo si kwa ajili ya kuvutia watalii
pekee bali kwa watu wote kwenye nyanja za Utamaduni, mila na desturi za
mwafrika kupitia njia ya muziki.
Simai pia amesisitiza
kwa vyombo vya habari na wataalamu wa teknolojia ya habari Nchini
kuendelea kuwaunga mkono katika kutangaza taarifa za habari za tamasha hilo
ikiwemo mandhari ya mji wa Zanzibar ili lionekane duniani kote na kuwatia hamu
wale ambao hawajawahi kufika Zanzibar kuamua kwenda kushuhudia.
Kwa upande wao Mabalozi wa Uswis na
Norway wanaoziwakilisha nchini zao hapa Tanzania, wamewapongeza Busara Promotions
kwa namna wanavyoendesha tamasha hilo ikiwemo kukuza tamaduni za Mwafrika
kupitia njia za Sanaa.
Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Bi.
Tinguely Mattli amesema wanaamini tamasha hilo ni moja ya njia ya kufikisha
ujumbe kwa wananchi kupitia wasanii ambao wamekuwa ni kioo cha jamii.
Nae Mwakilishi wa Balozi
wa Norway nchini na Mkuu wa Idara ya Ushirikiano, Trygve Bendiksby
alisema kupitia kauli mbiu ya mapambano dhdi ya rushwa ujumbe utafika kwa
wakati na haraka kupitia wasanii ambao jamii imekuwa ikiwafuatilia kwa ukaribu
hivyo wataendelea kudhamini tamasha hilo kwa kipindi kingine.
“Tunaungana na Busara Promotions
kwenye tamasha ili kubwa na tutaendelea kulidhamini tamasha kwa kipindi kipindi
cha miaka mitatu mingine” alisema Bendiksby.
Ubalozi huo wa Norway na Busara
Promotions wanatarajia kutiliana saini ya udhamini wa miaka mitatu mingine hapo
baadae. Tayari Norway imeweza kulidhamini tamasha hilo kwa muda wa miaka tisa
(9) kwa kipindi tofautitofauti.
Naye Mkurugenzi wa Busara Promotions,
Mahmoud Yusuf amesema kuwa, wamekuwa wakipokea maombi mengi ya
wasanii ndani na nje ambapo walio na sifa ndio wenye
kuchaguliwa kila mwaka ambapo kwa mwaka huu karibu wote waliochaguliwa ni wa
kiwango cha juu.
“Watu ni wengi na karibu hoteli zote
zenye hadhi ya nyota nne na tano hususan maeneo ya Mji Mkongwe zimejaa na
maeneo mengine watu wamejiandaa kwa ajili ya tamasha ili kubwa visiwani hapa”
alisema Yusuf.
Yusuf amesema kuwa, wenyeji wamepewa
nafasi ya kipekee ya kushuhudia tamasha hilo kwa bei ya ofa maalum kwa siku
tsh. 10,000 huku kwa siku zote nne akitakiwa kulipa tsh. 20,000 huku akitaka
pia wawe mfano wa kuigwa kwa kuonesha ukarimu na upendo kwa wageni kuanzia
vyombo vya usafiri maeneo ya mitaa na manunuzi ili wajisikie wapo na wenyeji
wenye moyo wa kupokea wageni.
Naye Meneja waTamasha hilo, Ramadhan
Journey alisema kuwa, kwa mwaka huu ni la 16 vikundi 44,
vinatarajia kuonesha burudani kwa siku nne kwenye majukwaa matatu
tofauti ya katika ukumbi wa kihistoria wa ‘Old Fort’ mjini Stone Town,
Zanzibar.
Aidha, Journey ametaja baadhi ya
orodha ya Wasanii kwa mwaka huu ni akiwemo: Fid Q kutoka Tanzania
Bara, Wasanii wengine na Nchi zao kwenye mabano ni pamoja na:
Mokoomba (Zimbabwe), Afrigo Band (Uganda), Fadhilee Itulya (Kenya), Ifrikya
Spirit (Algeria), Rajab Suleiman & Kithara ( Zanzibar), Tune Recreation
Committee, (Afrika Kusini), Ithrene (Algeria). Hoba Hoba Spirit (Morocco).
Pia wamo: M'Toro Chamou
(Mayotte/Reunion), Trio Kazanchis +2 (Ethiopia/Switzerland), Faith Mussa
(Malawi), Shamsi Music (Kenya), Sofaz (Reunion), Dago Roots(
Reunion), Lydol (Cameroun), Jackie Akello (Uganda), S Kide &
Wakupeti Band (Tanzania), Tausi Women's Taarab (Zanzibar), Mkubwa na Wanawe
Crew (Tanzania), Damian Soul (Tanzania) na Wamwiduka Band (Tanzania)
na wengineo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment