WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lihakikishe Tanzania inaibuka na ushindi katika fainali za michuano ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.
Mashindano ya mpira wa miguu kwa Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 barani Afrika (AFCON) yanayotarajiwa kufanyika mwaka huu nchini Tanzania.
Ametoa agizo hilo leo asubuhi (Alhamisi, Februari 7, 2019) Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge waKilolo, Venance Mwamoto.
Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali imeyahusishaje mashindano hayo ya AFCON na mkakati wa kuendeleza utalii nchini, ambapo Waziri Mkuu amesema maandalizi yote yanaendelea kufanyika na Serikali imejiandaa vya kutosha kupokea wageni hao.
Waziri Mkuu amesema TFF inaendelea na maandalizi ya mashindano hayo ya vijana chini ya umri wa miaka 17 baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kuipa Tanzania uenyeji wa fainali hizo.
Amesema Watanzania wanatakiwa wawe wazalendo na kuipa ushirikiano timu yao ili kuhakikisha inaibuka mshindi kwenye fainali hizo.
Pia Waziri Mkuu amesemaWizara ya Maliasili na Utalii itatumia mashindano hayo kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.“Tutawapeleka Kilwa wakaone majengo ya zamani yaliyokaliwa na Waarabu na maeneo mengine.”
Waziri Mkuu amewasihi Watanzania kutumia fursa ya mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika nchini kwa kufanya shughuli mbalimbali zitakazowaongezea kipato.“Kwa kupitia mashindano hayo sisi kama Watanzania tumejipanga huduma zote zipo , za Chakula, Hoteli na usafiri.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kazi kubwa ya kushawishi FIFA kuyaleta mashindano haya hapa nchini pamoja na ujio wa Rais wa FIFA, pia TFF kwa uratibu wa mashindano hayo sasa.
No comments:
Post a Comment