Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi lililofanyika tarehe 13 Februari, 2019.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo na Wawakilishi kutoka Taasisi za Wizara.
Na
Asteria Muhozya, Dodoma
Naibu wa Waziri wa Madini
Stanslaus Nyongo amewataka watumishi wa Wizara ya Madini kujiepusha na vitendo
vya rushwa ikiwemo kuzuia rushwa katika sehemu zao za kazi kwani suala hilo linasababisha
migogoro kwenye sekta ya madini.
Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo
Februari 13 wakati akifungua mkutano wa Baraza la wafanyakazi la wizara na
kuongeza kuwa, serikali inafuatilia mienendo ya watumishi wa sekta husika.
Alisema kuwa, wako watumishi
wanaomiliki leseni kwa dhuluma suala ambalo pia limechangia kuwepo kwa migogoro
mingi kwenye sekta na kueleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. Magufuli anasisitiza suala la kuzingatia maadili katika utumishi wa umma
na hususan katika sekta ya madini.
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri Nyongo alilitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhakikisha linajiendesha
kwa faida na kusisitiza kuwa Serikali inataka gawio.
Aidha, aliutaka uongozi wa STAMICO
kuzingatia maslahi ya watumishi kwa kutoa motisha mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuwapatia mafunzo lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi wa shirika kwa
ujumla.
Akizungumzia mafanikio makubwa
katika Sekta ya Madini, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa ni pamoja na
mabadiliko ya Sheria ya Madini na kusisitiza kuwa kwa Afrika Tanzania imekuwa
mfano kama nchi bora inayosimamia vyema rasilimali za madini.
“Sifa bora kwenye usimamizi wa
Sekta ya Madini zisitufanye tubweteke bali tuendelee kufanya kazi kwa ubunifu
wa hali ya juu huku tukizingatia maadili ya kazi,” alisema Nyongo
Nyongo aliendelea kusema kuwa,
kama moja ya mikakati ya kutoa motisha kwa watumishi, uongozi wa Wizara
unatakiwa kutoa fursa mbalimbali kwa watumishi ikiwa ni pamoja na mafunzo.
Wakati huo huo, akizungumza kwa
niaba ya watumishi, Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya
(TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Joyce Manyama alisema kuwa watumishi kupitia
chama chao watafanya kazi bega kwa bega na uongozi wa Wizara ili kuhakikisha
kuwa Sekta ya Madini inakuwa na viwanda vingi vya uongezaji thamani madini ili
kufikia malengo ya Serikali kupitia mchango wa Sekta ya Madini kwenye ukuaji wa
Pato la Taifa.
Aidha, Manyama alichukua fursa
hiyo kuishukuru Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Shirika la Vyama vya
Wachimbaji wa Madini Nchini (FEMATA), wachimbaji wadogo kwa kuitisha mkutano
uliofanyika hivi karibuni baina yao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Magufuli
Vilevile, aliishukuru Wizara kwa
kuanzisha mfumo mpya wa utunzaji wa kumbukumbu za Wizara unaojulikana kama Electronic Filing Management System
ambao utaboresha utunzaji wa kumbukumbu na kurahisisha upatikanaji wake pindi
zinapohitajika.
Pia, aliiomba Wizara kuendelea
kusimamia zoezi la upandishwaji wa vyeo ili watumishi waweze kupandishwa vyeo
kulingana na sifa wanazokuwa nazo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya
Madini, Profesa Simon Msanjila alisema kuwa Wizara itaendelea kuweka mazingira
mazuri ya kazi ili kila mtumishi afanye kazi kwa ubunifu zaidi.
Aliongeza kuwa, kwa sasa Wizara
inafanya vizuri ambapo Sekta ya Madini imekua kwa asilimia 18 huku mchango wa
sekta kwa fedha za kigeni ikiwa ya tatu nyuma ya Kilimo na Utalii na kueleza
kwamba, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna rushwa na kukosekana uadilifu.
No comments:
Post a Comment