Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo (wa pili kulia) wakati alipofanya ziara katika halamashauri ya wilaya ya Kwimba kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Senyi Ngaga.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua majalada katika masijala ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wakati wakati alipofanya ziara katika halmashauri hiyo kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Na Munir Shemweta, KWIMBA
Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline
Mabula ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza kuwapatia
viwanja ama fedha wananchi 44 waliotakiwa kupatiwa viwanja katika eneo la
Ngungumalwa wilayani humo ndani ya miezi mitatu na wasipotekeleza waliohusika
katika suala hilo watawajibishwa.
Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana tarehe 13 Januari 2019 katika
wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ulipaji
maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi katika kanda ya Ziwa.
Aidha, ameitaka halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kufanya uchunguzi
wa kiasi cha fedha takriban milioni 74 zilizotolewa na wananchi kwa ajili ya
kupimiwa na kupatiwa viwanja eneo la Ngungumalwa ambazo hazikutumika kwa kazi
hiyo ili kubaini zilitumika katika mazingira gani tofauti na malengo
yaliyokusudiwa.
Dkt Mabula alisema iwapo wananchi hao hawatapatiwa viwanja ama
kurudishiwa fedha zao ndani ya muda wa miezi mitatu aliotoa basi wote
waliohusika kwa namna moja ama nyingine watawajibishwa ili kurudisha imani kwa
wananchi.
‘’Kuchukua fedha za wananchi bila kupatiwa maeneo kunawafanya
kukosa imani na serikali yao na mimi sitakubali kuona wananchi wakidhulumiwa
haki yao na halmashauri ya Kwimba ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapatiwa
maeneo haraka iwezekanavyo’’ alisema Mabula.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kwimba Pendo Malabeja
alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Mkazi kuwa halmashauri
yake ilishaanza kuwalipa baadhi ya wananchi ingawa hakuainisha kiasi na idadi
ya wananchi waliolipwa na kubainisha kuwa suala hilo bado linaendelea kufanyiwa
kazi.
Vile vile, Dkt Mabula ameitaka halmashauri ya Wilaya ya Kwimba
kupanga na kupima maeneo yote ambayo yanakuwa kwa kasi na kuacha kujikita
katika zoezi la uarasimishaji ambapo alifafanua kitendo cha kuacha kupanga na
kupima maeneo yanayokuwa kwa kasi kutasabaisha ujenzi holela.
Aliongeza kuwa, Wilaya ya Kwimba iko nyuma sana katika kupima na
kupanga maeneo jambo linaloifanya halmashauri hiyo kushindwa kujikusanyia
mapato mengi kupitia sekta ya ardhi ambapo alitolea mfano wa jiji la Dodoma
kuwa limekuwa likoongoza katika ukusanyaji mapato ya serikali ambapo mengi
yanatokana na kupima na kuuza viwanja.
Ameitaka halmashauri hiyo kijipanga vizuri na kuitumia Ofisi ya
Ardhi Kanda ya Ziwa pamoja na halmashauri jirani kama Misungwi kusaidia katika
zoezi la kupima viwanja ili kuhakikisha linapanga na kupima maeneo mengi
sambamba na kuwa na mji uliopangika huku ikijiongezea mapato.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Senyi Ngaga alimueleza
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa wilaya yake ilikuwa
nyuma katika masuala ya ardhi lakini sasa wamejiwekea mkakati maalum
kuhakikisha inakuwa na maeneo mengi yalipangwa na kupimwa na suala la kwanza ni
kuhakikisha idara ya ardhi inapatiwa fedha ya kutosha kwa nia ya kufanya kazi
zake kwa ufanisi.
MWISHO
No comments:
Post a Comment