Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine (kushoto) akihimiza jambo kuhusu ushirikiano wa pamoja kati ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula katika kuchagiza mnyororo wa thamani wa mahindi nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine (katikati kushoto) akizungumza na ugeni kutoka NFRA walioongozwa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Bi Vumilia Zikankuba (katikati kulia) kuhusu mkakati wa kuimarisha mnyororo wa thamani wa mahindi nchini.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Bi Vumilia Zikankuba akizungumza wakati wa kikao hicho.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) zimekuja na
mkakati kabambe unaolenga kuimarisha mnyororo wa thamani wa mahindi ili kuleta
tija na kuwawezesha wakulima wadogo wadogo wa zao hilo hapa nchini kwa kuwapatia
soko la uhakika la mazao yao.
Mkakati huo wa pamoja unalenga
kupunguza changamoto za ukosefu wa soko la uhakika la zao la mahindi ambazo
zimekuwa zikiwakabili wakulima wa zao hilo hapa nchini.
Mkakati huo umewekwa wazi na
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine mara baada ya kikao cha pamoja
kilicholenga kujadili namna bora ya kuwanyanyua wakulima wadogo wadogo wa zao
la mahindi kupitia ununuzi zao hilo kupitia NFRA.
“Tumekubaliana na NFRA kuja na
mpango wa mkakati utakaosaidia kuimarisha mnyororo wa thamani wa mahindi ili
kuongeza tija kwenye masoko ili kuwaondolea wakulima wadogo wadogo changamoto
za masoko ya mahindi yanayowakabili kwa sasa,” alisema Bw. Justine.
Akizungumzia nafasi ya TADB katika
kuchagiza uwekezaji katika mnyororo mzima wa ongezeko la thamani wa zao la
mahindi, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA), Bibi Vumilia Zikankuba, amesema utayari wa Benki ya Maendeleo ya
Kilimo katika kusaidia zao la mahindi utasaidia kwa kiwango kikubwa uhakika wa
soko na hivyo kuwawezesha wakulima wadogo wadogo wa zao hilo hapa nchini.
“Fursa za mikopo ya TADB inatupa
nafasi ya kujipanga kimakakati kwa ajili ya kupata mtaji wa uhakika wa
uendeshaji wa shughuli zetu za kununulia mahindi yenye ubora hivyo kuwa na
uhakika wa soko kwa mazao ya wakulima,” alisema.
No comments:
Post a Comment