Thursday, January 17, 2019

RC Wangabo azihamasisha Taasisi kufika TFS kuchukua miti ya kupanda bure


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo akiwa katika kitalu cha miti cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kilichopo Manispaa ya Sumbawanga akikagua miti ya mbao iliyotengwa kwaajili ya taasisi na wananchi kuweza kupatiwa. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo (kulia) pamoja na baadhi ya wataalamu wa ofisi yake walipotembelea moja ya vitalu vya miti vilivyopo manispaa ya Sumbawanga siku chache kabla ya kilele cha upandaji miti Kimkoa tarehe 19.1.2019
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo akimhoji Peter Mazigo kiongozi wa taasisi ya vijana (FECEE) inayojishughulisha na uuzaji wa miti ya mbao na matunda waliopo manispaa ya sumbawanga juu ya mwitikio wa wananchi katika ununuzi wa miti.

Katika kuelekea siku ya upandaji miti kimkoa ambayo hufanyika kila tarehe 19 ya mwezi wa kwanza kila mwaka Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa wananchi pamoja na taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali kufika katika ofisi za wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) zilizopo kijiji cha mponda kata ya Majengo, manispaa ya Sumbawanga ili kuweza kupatiwa miche ya miti na kuweza kuipanda katika maeneo yao.

Amesema kuwa TFS wametenga miche 100,000 kwaajili ya kutoa bure kwa taasisi pamoja na wananchi ambao watachangia kiasi cha shilingi 150 kwa mti mmoja na kuongeza kuwa kuchukua miti hiyo na kuipanda kutaiwezesha taasisi ama mwananchi kuwekeza katika miti, kupendezesha eneo lake hali itakayopelekea kupendezesha mandhari ya mkoa kwa ujumla.

“Uchukuaji wa miti hii umekuwa unasuasua basi nichukue nafasi hii nitoe wito kwa wananchi wote wa mkoa wa rukwa na hasa wa mazingira haya ya manispaa ya Sumbawanga, waje kuchukua miti, miti ambayo imekwishachukuliwa mpaka sasa haizidi miche 25,000 kwahiyo tuna zaidi ya miche 75,000 ambayo inangoja kuchukuliwa kama inavyoonekana hapa,” Alisema.

Ameyasema hayo alipotemnbelea vitalu vya miche vilivyovyopo katika hifadhi ya msitu wa mbizi wenye eneo la hekta zaidi ya 4000 na kukuta miche hiyo iliyopangwa kugaiwa kwa taasisi na wanachi ikiwa bado ipo na haina mchukuzi.

Halikadhalika Mh. Wangabo alitembelea vitalu vya vikundi vya vijana ambao wanajishughulisha na biashara ya miti ya matunda pamoja na miti ya mbao ili kujua hali ya biashara hiyo ilivyo na muitikio wa wananchi ma mkoa wa Rukwa pamoja na muitikio wa halamashauri katika upandaji wa miti  tangu kuanza kuhamasisha zoezi hilo.

Mmoja wa vijana wanaoshughulika na uuzaji wa miti Peter Mazigo aliwaasa wananchi wa mkoa wa Rukwa kupanda miti aina ya miparachichi ambayo inafaa kupandwa katika mkoa wa Rukwa na kuleta mafanikio.

Ziara hiyo ya kutembelea vitalu imetokana na maelekezo aliyoyatoa hivi karibuni kwa halmashauri juu ya uwepo wa idadi ya miti anazokuwa anasomewa kila ifikapo siku ya kupanda miti kimkoa, takwimu ambazo halmashauri hizo zinashindwa kuthibitisha uwepo wa miti hiyo na matokeo yake kuonekana kuwa ni uwongo na hivyo kuagiza kuwa takwimu zinazotakiwa zitokane na vitalu vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya mkoa. 

No comments:

Post a Comment