Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Mji wa Serikali katika eneo la Ihumwa
jijini Dodoma, Januari 17, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Saidi Kiwape
(kushoto) ambaye ni fundi wa kusuka nondo wakati alipokagua ujenzi wa Jengo la
Ofisi za Wizara ya Nishati kwenye eneo la Ihumwa unapojengwa Mji wa
Serikali jijini Dodoma, Januri 17, 2019. Wapili kulia ni Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani, watatu kulia ni Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri
Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Ataka kampuni ya Mzinga Holdings isimamiwe kwa
karibu
*Ahimiza tarehe ya mwisho ni Januari 31, mwaka huu
ZIKIWA zimepita siku 20 tangu akague ujenzi wa mji
wa Serikali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na ujenzi
unaoendelea katika eneo la Mji wa Serikali lililoko Ihumwa.
Hata hivyo, amesema kampuni ya ujenzi ya Mzinga
Holdings inahitaji kusimamiwa kwa karibu zaidi ili ikamilishe ujenzi wa majengo
yake kabla ya Januari 31, mwaka huu. “Nitakuja kukagua kazi na kupokea funguo
za ofisi siku hiyo,” amesema.
Ametoa kauli hizo leo mchana
(Alhamisi, Januari 16, 2019) mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za wizara
zote pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Ihumwa
lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.
Waziri Mkuu ambaye alianza kukagua ujenzi kwenye
Ofisi ya Makamu wa Rais, ametembelea majengo ya wizara zote na kubaini bado
kuna changamoto zinazojitokeza kutokana na utendaji wa mazoea miongoni mwa
watumishi wa Serikali.
Akiwa katika jengo la Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Waziri Mkuu alipokea malalamiko kutoka kwa meneja mradi, Bi.
Selemina Rwehumbiza kwamba aliandaa certificate tangu tarehe
13 Januari lakini hadi sasa hajapata malipo. Alipofuatilia, alijibiwa na
mshauri mwelekezi kwamba wamepokea certificate hiyo jana jioni
(Jumatano, Januari 16, 2019).
“Kama kazi hii muhimu ya Mheshimiwa Rais, na
anayesimamia ni Waziri Mkuu inacheleweshwa hivi, je akija mwananchi wa kawaida
huko ofisini kwenu atachukua muda gani kupatiwa huduma?,” Waziri Mkuu alimhoji
Mshauri Mwelekezi wa mradi huo kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Mhandisi
Hilary Msaki.
“Huu ni mfano halisi wa malalamiko yanayotoka huko
nje kwamba Serikali haijibu barua za wananchi. Sasa nyaraka kutoka hapa Mtumba
inachukua wiki nzima kwenda mjini, na mtu bado hajajibiwa. Sielewi ni kwa nini
barua iende hadi mjini, wakati wakandarasi wako huku. Kwa nini ninyi msipokee
hizo nyaraka na kuzikimbiza mjini kisha mrudishe majibu hapa site?”,
alihoji Waziri Mkuu.
“Kuanzia sasa, kazi zote mpokee ninyi, na ninyi
ndiyo mzipeleke huko mjini na kurudi na majibu hapa site kwa
wateja wenu, kwani wakandarasi wote wako hapa,” alisisitiza.
Akiwa katika eneo la Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri Mkuu alielezwa na Waziri Ummy Mwalimu
kwamba wana changamoto ya kutopatiwa taarifa za maendeleo ya mradi. “Tangu
mradi unaze hatujapewa taarifa hata moja, wakurugenzi wapo wanakuja, lakini
mshauri mwelekezi hatupi ripoti yoyote juu ya huu mradi,” alisema.
Alipohoji ni kwa nini taarifa hazitolewi, Waziri
Mkuu alibaini kuwa hata watu wa TEMESA pia hawakuwepo kwenye zoezi hilo la
ukaguzi. “Niliagiza TBA wahamie hapa, nao wameweka ofisi yao hapa hapa.
Nimeulizia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wako wapi, nikaambiwa wako mjini.
Ni kwa nini hawako hapa?” alihoji.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa tangi la
maji lenye ujazo wa lita milioni moja, Waziri Mkuu alisema pamoja na spidi
anayoihimiza, bado wakandarasi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia ubora
unaotakiwa (quality).
Alisema kwa ujumla kazi nyingi zimeboreshwa tangu
alipokagua mradi huo Desemba 27, mwaka jana. Aliitaka TBA kwa kushirikiana na
Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma na Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa/Mkurugenzi wa Dodoma wawasimamie wakandarasi na hasa wale wa Mzinga ili
kazi yao ikailike kwa wakati.
“Nimesisitiza katika kila site, zile
kazi ndogondogo zisizohitaji ujuzi au ufundi mkubwa, zigawiwe kwa vijana ili
kuongeza kasi lakini tuzingatie ubora wa kazi,” alisisitiza.
Desemba 27, mwaka jana, Waziri Mkuu alikagua ujenzi
wa eneo la Mji wa Serikali na kubaini kuwa baadhi ya wakandarasi hawaendi na
kasi inayotarajiwa na Serikali. Siku iliyofuata aliitisha kikao cha Mawaziri
wote, Makatibu Wakuu na wakandarasi wao ili waeleze kazi hiyo itakamilishwa
lini. Kikao hicho alikifanyia hukohuko Ihumwa.
No comments:
Post a Comment