Thursday, January 17, 2019

RC Wangabo asisitiza ushirikiano baina ya watendaji wa ngazi zote kutatua changamoto za elimu


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi, kuhakikisha kila mtumishi kwa nafasi yake na majukumu yake anashirikishwa katika kutatua changamoto za wananchi ikiwemo elimu, afya, maji na kilimo pamojana kushirikiana na wananchi kutatua chnagmoto hizo.
Amesema kuwa ili kutatua hayo halmashauri inapaswa kuongeza vyanzo vya mapato ikiwemo kuzidisha malengo ya makusanyo kwa mwaka ili kuweza kukabiliana na changamoto anazokuwa anasomewa kila anapofanya ziara katika shule mbalimbali za halmashauri na kumuomba achangie kutatua changamoto zao.
“Mpige hesabu zote muwarudishie huko jamii ili jamii iguswe kwamba alaa! Kumbe kuna changamoto kubwa sana zisingoje sisi viongozi ambao pengine hatuna nafasi ya kuzunguka sekondari zote, lakini kama tutafanya hivi tutaondoa changamoto zote hizi na matatizo na haya yote mliyoyasema yako chini ya uwezo wenu, sio mambo ya mkuu wa mkoa haya, ni mambo ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi, kata na vijiji vyenu, kama ni “support” tunatoa ya kuhamasisha,naweza kusema nanunua bati mbili tatu, je, ninatatua matatizo yote hayo?”Alibainisha.
Ameongeza kuwa kazi ya shule ni kuandaa taarifa nzuri na kuikabidhi kwa watendaji wa halmashauri kuanzia Mtendaji wa kata na vijiji pamoja na viongozi wa kisiasa akiwemo diwani wa kata husika ili taarifa hizo ziwafikie wananchi watambue kupitia vikao vya kamati ya maendeleo ya kata ambao ni mfumo mzuri uliowekwa na serikali katika kutambua changamoto na kuzitatua.
Ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya shule ya sekondari Chala, iliyopo kata ya Chala Wilayani Nkasi na mkuu wa shule hiyo Fatma Mchomvu aliyemuomba kufanya harambee ya haraka kutoka kwa msafara alioambatana naoi li kuweza kukarabati nyumba ya “Matron” ambapo hadi wanafikisha ombi hilo waalimu walikwishajichangisha shilingi 50,000/-.
“Walimu wamejitolea kuchangia 50,000/- kusaidia kukarabati nyumba moja ya mwalimu ya “matron” kwasababu kule wanafunzi wako peke yao hakuna ulinzi kwahiyo nao wakaomba kupitia msafara wako, na wewe ndio kiongozi wetu tupate harambee ya haraka ili angalau tuanze kufanya ukarabati wa jengo hilo ili angalau wanafunzi wawe salama kwasababu wanakaa mbali na hakuna mlezi wa kukaa nae kule,” Alifafanua.

No comments:

Post a Comment