Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo
amewataka wajasiliamali wote mkoani humo kujitokeza kupatiwa vitambulisho vya
ijasiliamali vilivyotolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa mikoa na wilaya
zote nchini ili kuwaepusha wajasiliamali hao na bughudha wanazozipata katika
kuendesha biashara zao za kila siku.
Amesema kuwa kila halmashauri kati ya
halmashauri nne za mkoa wa Rukwa ilipatiwa vitambulisho 6,250 katikati ya mwezi
Disemba mwaka 2018 lakini hadi kufikia leo katikati ya mwezi wa kwanza
vitambulisho vilivyogawiwa havizidi 150 kwa mkoa mzima hali iliyopelekea Mh.
Wangabo kuahirisha ziara ya siku nne aliyopanga kuifanya katika halmashauri ya
Wilaya ya Kalambo ili kujionea miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Nawataka waende katika halmashauri zote
haraka iwezekanavyo vinginevyo watakosa hii nafasi ya kuapata vitambulisho na
kitakachofuata kinaweza kisiwe kizuri kwa wajasiliamali, kwasababu hiki ni
kitambulisho ndicho kinachomfanya mjasiliamali huyu mdogo atambulike na
asibughudhiwe kama mheshimiwa rais alivyosema, sasa usipopata kitambulisho
maana yake ni kinyume chake ndicho kitakachokuja, unapata kitambulisho ili
usibughudhiwe, lakini wewe hujapata kitambulisho inamaana utabughudhiwa, mimi
nisingependa wajasiliamali wapate bughudha,” Alibainisha.
Ameyasema hayo baada ya kupata taarifa ya
Wilaya ya Kalambo juu ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo, mapokezi ya
wanafunzi wa kidato cha kwanza, ukusanyaji wa mapato na matumizi ya
halmashauri, ugawaji wa vitambulisho hivyo pamoja na hali ya kilimo ya Wilaya
kabla ya kutaka kuanza ziara yake katika wilaya hiyo.
Aidha amesisitiza kuwa tathmini ya ugawaji wa
vitambulisho hivyo itafanyika baada ya siku kumi tangu leo tarehe 15.1.2019
hadi tarehe 25.1.2019 ili kuona muitikio wa wajasiliamali hao kwa halmashauri
zote na kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri hizo kuhakikisha wanaongeza kasi
ya kuwasajili na kuwakabidhi wajasiliamali hao vitambulisho vyao bila ya
bughudha yoyote.
Wakati akiwasilisha taarifa ya wilaya, katibu
tawala wa wilaya ya Kalambo Frank Sichalwe alisema kuwa tangu kufanyika kwa
uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho hivyo mwanzoni mwa mwaka huu ni
wajasiliamali kumi tu ndio waliopatiwa vitambulisho hivyo pamoja na kuendelea
na hamasa ya kuwatambua wajasiliamali wengine.
“Zoezi la hamasa na ugawaji wa vitambulisho
linaendelea ili vitambulisho vingi zaidi viweze kutolewa na kuwanufaisha
wajasiliamali katika sekta isiyorasmi kama mheshimiwa Rais alivyokusudia, mpaka
sasa Ulumi tumepata wajasiliamali 80, Mwimbi 30, Kasanga 30, Mwazye 20 na Matai
wamejitokeza wajasiliamali zaidi ya 100 mpaka sasa,” Alisema.
Vitambulisho vya ujasiliamali viligagiwa kwa
wakuu wote wa mikoa 26 mwanzoni mwa mwezi Disema mwaka 2018 na kila mkoa kupata
vitambulisho 25,000 ili kuweza kuvigawa kwa wakuu wa wilaya na hatimae kufika
mikononi mwa wakurugenzi ili kuwapatia wahusika wa vitambulisho hivyo kwa lengo
la kupunguza bughudha kwa wajasiliamali wataopata vitambulisho hivyo vyenye
gharama ya shilingi 20,000 kwa kila kitambulisho.
No comments:
Post a Comment