Na
Stella Kalinga, Simiyu
Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Bashiru Ally amewataka Watumishi
wa Serikali kujifunza kufanya maamuzi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kwa ajili ya maslahi
mapana ya Taifa.
Dkt. Bashiru
ameyasema hayo mjini Bariadi katika kikao na Wakurugenzi wa Taasisi
zitakazoshirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko
wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kujenga kiwanda cha (vifaa tiba) bidhaa za afya
zitokanazo na pamba wilayani Bariadi, baadhi ya viongozi, watendaji wa Chama na
Serikali na wawekezaji katika zao la pamba mkoani Simiyu, ambacho
kililenga kujadili ujenzi wa kiwanda hicho na mnyororo wa thamani wa zao la
pamba.
Dkt.
Bashiru amesema watumishi wa serikali waache tabia ya kuzungumza bila
kutenda badala yake wawe na moyo wa uzalendo na wafanye maamuzi sahihi kwa muda
muafaka huku akisisitiza kuwa hawapaswi kuwa sehemu ya vikwazo katika
maamuzi ya utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo.
“Watumishi
wa Serikali jifunzeni kutoka kwenye tabia ya Rais wetu, fanyeni
maamuzi kwa maslahi mapana ya Taifa, muwe na moyo wa uzalendo na ujasiri katika
kuchukua maamuzi; maamuzi hayo yafanyike kwa usahihi kwa muda muafaka” alisema
Dkt.. Bashiru.
Kuhusu
ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za afya zinazotokana na zao la pamba mkoani
Simiyu, Dkt. Bashiru alioneshwa kutoridhishwa na kasi ya maandalizi ya ujenzi
huo na kumwagiza Mkurugenzi wa kituo cha uwekezaji (TIC), Bw.
Godfrey Mwambe kuratibu mazungumzo ya kuwakutanisha wahusika wote ili
utekelezaji wa mradi uanze mara moja.
“Tulikubaliana
kazi itaanza Desemba 2018 na Desemba imeshapita, tumedhamiria na tumeshatamka
kuwa tutajenga viwanda, hatuwezi tukakwamisha mipango ya kujenga viwanda na
wakati tumeamua kujenga uchumi wa viwanda hapana; Tarehe 09 Januari saa 3:00
asubuhi wale wote wanaohusika na ujenzi wa kiwanda hiki tukutane Lumumba
tuzungumze” alisema Dkt. Bashiru.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema ni vema viongozi
wa Serikali wanaohusika katika kutoa maamuzi yatakayopelekea ujenzi wa kiwanda
cha bidhaa za afya zitokanazo na pamba wachukue
hatua, ili ujenzi uanze mara moja na wamiliki wa viwanda vya
kuchambua pamba waanze kujua mahitaji ya pamba itakayotumika na kiwanda hicho
katika msimu wa mwaka 2018/2019.
“Yapo
mambo tulikubaliana kufikia Desemba 2018 yawe yamekamilika, tunaomba kama kuna
mambo bado yako mezani yaondoke jambo hili liweze kusogea, taratibu za manunuzi
zianze ili hatua za kutengeneza mashine zifanyike na kupitia pamba itakayoanza
kununuliwa mwezi Mei, wamiliki wa viwanda vya kuchambua pamba waanze kujua
mahitaji ya kiwanda katika msimu wa mwaka 2018/2019, ili kiwanda kisije
kikakamilika pamba ikakakosekana” alisema Mtaka.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Bw. Marco Mtunga amesema upatikanaji
wa malighafi ya kiwanda cha vifaa tiba (bidhaa za afya zitokanazo na zao
la pamba) kinachotarajiwa kujengwa Bariadi ni wa uhakika na
kubainisha kuwa Bodi hiyo imejiwekea malengo ya kuzalisha tani milioni moja
ifikapo mwaka 2022.
Mkurugenzi
wa Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF), Bernad Konga amesema tayari
bodi ya mfuko huo imeshatenga kiasi cha shilingi bilioni kumi kwa ajili ya
kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha (vifaa tiba) bidhaa za afya
zitokanazo na pamba mkoani Simiyu, lengo likiwa ni kupunguza gharama za kuagiza
bidhaa hizo nje ya nchi na kuongeza thamani ya zao la pamba nchini.
Mkurugenzi
Mkuu wa Bohari ya Dawa(MSD), Bw. Laurian Rugambwa amesema bidhaa za afya
zitokanazo zao la pamba zitakazozalishwa na kiwanda hicho zitapata soko la
uhakika katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa
Jangwa la Sahara(SADC) na hapa nchini kupitia Bohari hiyo, kwa kuwa sasa bidhaa
hizo zinaagizwa nje ya nchi.
Baadhi
ya wawekezaji wa viwanda vya kuchambua pamba mkoani Simiyu wamesema pamoja na
kujenga kiwanda cha bidhaa za afya zitokanazo na pamba njia kuu ya kuongeza
thamani ya zao la pamba ni kujenga viwanda vya nyuzi na nguo, huku wadau wa
wakitoa maoni yao
.
“Tunapaswa
kuongeza thamani ya zao la pamba ili wakulima waweze kunufaika na uzalishaji
wanaofanya, moja ya njia kuu ya kuongeza thamani ni uwekezaji katika viwanda
vya nyuzi na nguo, huu ni uwekezaji mkubwa unaotoa ajira nyingi, Serikali
ingalie upya sera, sheria na kodi zinazogusa uwekezaji katika eneo hili”
alisema Salum Khamis mwekezaji Shinyanga.
“Ipo
haja ya kwenda kwenye uwekezaji katika viwanda vya nyuzi na nguo hapa
nchini na kwa sababu sisi ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa
pamba Afrika, tukitegemea sana soko la nje kwa siku zijazo tunaweza kukwama
hasa katika suala bei ya pamba” alisema Boaz Ogola Kiwanda cha Kuchambua pamba
cha Alliance Ginnery.
Kiwanda
cha Bidhaa za afya zitokanazo na zao la pamba kinatarajiwa kujengwa mwaka huu
2019 katika Kata ya Dutwa wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu na Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), ambapo ujenzi huo
umeshirikisha Taasisi nyingine za Umma ambazo ni wadau muhimu katika
kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi.
Taasisi
hizo ni Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO), Shirika la Viwango
Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Benki ya Uwekezaji Tanzania
(TIB Corporate) na Bohari ya Dawa ya Taifa (MSD).
MWISHO
No comments:
Post a Comment