Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko
(wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Umma.
Pamoja na wachimbaji wadogo wa madini waliohudhuria mafunzo yanayotolewa na
wizara ili kuboresha utendaji wao.
Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amewataka
wachimbaji wadogo wa madini kuwa wazalendo na waaminifu kwa nchi kwa kulipa
kodi stahiki zinazotokana na biashara ya madini wanayoifanya.
Biteko amesema anashangazwa kuona kuwa mchango
wa wachimbaji wadogo katika pato la taifa ni mdogo ilihali asilimia 96 ya
shughuli za uchimbaji zinafanywa na wachimbaji wadogo na asilimia nne tu
zimeshikwa na wachimbaji wakubwa na ndio wanachangia Zaidi katika ukuaji wa
pato la taifa.
Biteko amebainisha kuwa hayo ni matokeo ya
ukwepaji wa baadhi ya wachimbaji wadogo katika kulipa kodi stahiki zitokanazo
na uchimbaji wa madini.
Ameyasema hayo leo tarehe 2 Januari, 2019
wakati akifungua rasmi mafunzo kwa wachimbaji
wadogo katika eneo la Katente mkoani Geita.
Akifungua mafunzo hayo, Biteko amesema, mnamo
mwaka 2016 Serikali ilitenga kiasi cha dola za kimarekani 3,703,630 kwa ajili
ya utafiti wa kina wa jiosayansi chini ya mradi wa Usimamizi Endelevu wa
Rasilimali Madini (SMMRP) ili kuboresha maisha ya mchimbaji mdogo na kutatua
changamoto zinazomkabili ikiwa ni pamoja na uzalishaji mdogo na uchimbaji
usiozingatia usalama na afya kwa mchimbaji.
Biteko alibainisha kuwa kazi ya utafiti katika
mji wa Katente umekamilika kama inavyoshuhudiwa kupitia mafunzo yanayotolewa
kwa wachimbaji wadogo wa eneo hilo yatakayosaidia kupunguza upotevu wa muda,
uharibifu wa mazingira, upotevu wa mitaji pamoja na upotevu wa madini ya
dhahabu yanayotokana na uelewa wa namna ya kufanya kazi hiyo.
Aidha, Biteko alibainisha kuwa, Baada ya
matokeo ya utafiti huo uliofanywa kwa ushirika baina ya Taasisi ya Jiolojia na
Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika
la Madini la Taifa (Stamico) na kubaini changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo
katika kukua kiuchumi.
Kutokana na changamoto zilizobainishwa na
utafiti huo, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeanza kujenga madarasa na
kufunga mitambo kwa ajili ya mafunzo Zaidi na kubainisha kuwa eneo la Katente
ni moja kati ya maeneo ambayo mafunzo hayo yatatolewa.
Pamoja na kupewa mafunzo hayo, Biteko
amewataka wachimbaji hao kuunda vikundi na kufanya shughuli zao ndani ya
vikundi ili kuirahisishia Serikali kuwatambua na kuwapa huduma stahiki
zitakazowawezesha kuboresha kazi zao pamoja na afya zao.
Akizungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali
katika kuboresha sekta ya uchimbaji mdogo; Biteko alisema ni pamoja na
kuendelea kutenga maeneo maalaum kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kutoa ruzuku,
kurahisisha utoaji wa leseni, pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara ili
kuwapa wachimbaji wadogo uelewa katika shughuli ya uchimbaji.
Utafiti huo ulifanyika kufuatia nia na adhma
ya Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais Dr. John Pombe Magufuli katika
kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanaondokana na uchimbaji usio na tija na
kwenda kwenye uchimbaji utakaoongeza kiasi cha uzalishaji na baadaye kuongeza
kipato kwa wachimbaji wadogo na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Huduma za
Jioloji kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Maruvuko
Msechu alisema mafunzo yanayofunguliwa ni matokeo ya dhamira ya Serikali ya
Awamu ya Tano yenye lengo la kuhakikisha watanzania wanafaidika na uwepo wa
madini nchini ili kujiondoa katika lundo la umaskini kwa kuongeza kipato na
kuimarisha sekta mtambuka za uchumi.
Msechu alisema, Utafiti huo ulifanyika katika
maeneo ya Ngazo, Kereza, na Katente wilayani Bukombe ukihusisha matumizi ya
taaluma ya jiolojia, jiofizikia, na jiokemia ukihusisha uchukuaji wa sampuli
mbalimbali za udongo na miamba.
Msechu aliongeza kwa kusema kuwa matokeo ya
utafiti huo yalipelekea kufanyika kwa utafiti wa kina katika eneo la Katente,
utafiti ulioanza rasmi tarehe 28 mwezi Oktoba, 2016 ambao ulipelekea jumla ya
chorongo 19 za DD na 24 za RC kuchorongwa na kukusanya jumla ya sampuli 2821.
Aidha aliushukuru uongozi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Bukombe, Mkuu wa Wilaya pamoja na kamati ya ulinzi ya wilaya ya
Bukombe kwa ushirikiano waliouonesha kipindi chote cha kufanya utafiti huo.
No comments:
Post a Comment