Saturday, December 1, 2018

MHE HASUNGA ATOA MIEZI SABA KWA TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO-TARI NA CHUO CHA KILIMO NALIENDELE KUWEKA ALAMA ZA MIPAKA YA ARDHI

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua mti wa Korosho zinazozalishwa kwa ajili ya mbegu katika Kituo cha Utafiti wa kilimo TARI-Naliendele Mkoani Mtwara wakati akiwa katika ziara ya kikazi tarehe 1 Disemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua mche wa Korosho unaozalishwa katika Kituo cha Utafiti wa kilimo TARI-Naliendele Mkoani Mtwara wakati akiwa katika ziara ya kikazi tarehe 1 Disemba 2018, Wengine pichani kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe Evod Mmanda na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti TARI-Naliendele Dkt Fortunatus Kapinga (Kulia).
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua akikagua shamba darasa kwa ajili ya korosho katika Kituo cha Utafiti wa kilimo TARI-Naliendele Mkoani Mtwara wakati akiwa katika ziara ya kikazi tarehe 1 Disemba 2018.
Miche ya korosho katika Kituo cha Utafiti wa kilimo TARI-Naliendele Mkoani Mtwara ikiwa katika kitalu nyumba (Green House) kabla ya kupelekwa kwa wakulima.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara

Uongozi wa Kituo cha Utafiti wa kilimo cha TARI-Naliendele na Chuo cha Kilimo Naliendele umepewa miezi saba kuanzia Disemba mosi mwaka huu 2018 mpaka mwezi Juni 2019 kuweka alama ya mipaka ya kudumu (Beckon) kwenye maeneo yao yote.

Agizo hilo limetolewa tarehe 1 Disemba 2018 na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akizungumza kwenye kikao cha kazi akiwa katika ziara ya kikazi katika Kituo na Chuo hicho Mkoani Mtwara.

Mhe Hasunga amepiga marufuku kwa wananchi kuingia katika maeneo hayo kwa kufanya shughuli yoyote kwani eneo hilo ni maalumu na limetengwa kwa ajili ya chuo na kituo hicho cha utafiti.

Alisema kuwa Kituo cha utafiti TARI-Naliendele kinaongoza kwa utafiti wa mbegu za mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na korosho ambayo inatoa mchango mkubwa Duniani hivyo ni lazima kujikita katika kuandika miradi mbalimbali ya kutafuta fedha katika Taasisi za ndani na nje ya nchi.

“Mkipata miradi na fedha za kutosha utafiti wenu utaimarika na kurahisisha huduma za utekelezaji wa majukumu yenu ikiwa ni pamoja na kuimarisha utafiti” Alisisitiza

Vilevile amewataka kusimamia vizuri miradi iliyopo kwa kuongeza uzalishaji na tija ili kuingiza kipato kitakacho rahisisha utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kuimarisha Taasisi na Chuo hicho kujitegemea.

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI-Naliendele kuongeza kasi ya utafiti ili kuyakabili magonjwa mbalimbali ya mazao yanayojitokeza mashambani kwa wakulima nchini.

Akijibu risala za chuo na Taasisi hiyo kuhusu upungufu wa watumishi, Waziri Hasunga alisema kuwa katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili serikali ilikuwa inafanya uhakiki wa watumishi hewa na wenye vyeti feki hivyo upungufu ulisababishwa na kubainika kwa watumishi hao walioondolewa kazini.

Hata hivyo baada ya kukamilika kwa zoezi hilo serikali ilitoa ruhusa ya kupanishwa madaraja kwa watumishi wote ambao walikuwa hawajapandishwa madaraja.

Aidha, Mhe Hasunga amewataka wafanyakazi wote wa Chuo cha Itafiti wa Kilimo na Kituo cha Utafiti TARI-Naliendele kufanya kazi kwa umoja na mshikamano huku akisisitiza zaidi kuhusu uwajibikaji, nidhamu na weledi.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment