Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameliomba Kanisa la Kiinjili na Kilutheri
Tanzania (KKKT) kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo na huduma
mbalimbali za jamii mkoani hapa.
Mtaka
ameyasema hayo Novemba 25, wakati alipozungumza na waumini wa Kanisa hilo
katika Usharika wa Tumain Bariadi Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa
Victoria, ambapo alikuwa mgeni rasmi katika harambee ya ujenzi wa vyumba vitano
vya madarasa na matundu 10'ya vyoo katika Shule Awali na Msingi ya Tumaini
(Tumaini Pre & Primary School) inayomilikiwa na kanisa hilo.
Amesema
kanisa hilo limekuwa na mchango mkubwa katika miradi mingi ya maendeleo
hususani katika sekta ya elimu, afya, maji na maeneo mengine muhimu ikiwemo
sekta ya fedha ambapo Kanisa hilo linamiliki Benki ya Maendeleo.
"Pamoja
na mradi huu wa shule ya msingi, tunaendelea kuliomba Kanisa kuona umuhimu wa
kuwekeza katika miradi mingine ya maendeleo kwenye mkoa wetu; Kanisa lina
hospitali, benki na vyuo vikuu; huu ni mkoa ambao bado haujawa na vyuo vikuu
vingi kwa hiyo ipo nafasi kwa kanisa kuona kama linaweza kuwa na chuo cha
ufundi, chuo cha kati au Tawi la Chuo Kikuu au kuwekeza katika eneo jingine
."alisema Mtaka.
Aidha,
amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania kwa kuwa limekuwa sehemu ya mafanikio ya nchi yetu tangu
imepata uhuru, kwani wapo Viongozi na Watanzania wengi katika maeneo tofauti
nchini ambao wamepata elimu katika Vyuo na shule za kanisa, huku akisisitiza
kanisa kuendelea kuombea amani na mshikamo wa nchi.
Naye
Askofu wa KKKT, Dayosis ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Dkt. Emmanuel
Makala amesema Kanisa litaendelea kushirikiana Serikali katika kuwafanya
watu.wamjue Mungu na kuwaletea wananchi maendeleo, ambapo amebainisha kuwa
ujenzi wa shule ni moja ya njia za kushirikiana na Serikali katika kuondoa
ujinga na kujenga Taifa lenye watu walioelimika jambo ambalo litairahisisha
Serikali katika kuwaongoza wananchi wake.
"Kanisa
litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha watu wa Simiyu katika wilaya
zote wanamjua Mungu; tunajenga shule ili tuondoe ujinga watu waelimike, ujinga
ukiondoka hata Serikali inapata nafuu kuwaongoza watu wake" alisema Askofu
Makala.
Awali
akisoma risala kwa mgeni rasmi, Katibu wa Kamati ya Ujenzi, Mwl. Oberlin Kileo
amesema ujenzi wa Shule ya Tumaini ulianza mwaka 2012, ambapo jumla ya vyumba
vya madarasa tisa, matundu ya vyoo 10, jiko, stoo na viwanja vya michezo
vilijengwa na kugharimu shilingi milioni 200 zikijumuisha na gharama za uwekaji
wa miundombinu ya maji na umeme.
Ameongeza
kuwa ili kujenga vyumba vya madarasa vitano na matundu 10 ya vyoo vivyokusudiwa
kujengwa kwa awamu ya pili jumla ya shilingi milioni 120 zinahitajika.
Katika
harambee hiyo jumla ya shilingi 41,526,500/= zilipatikana, kati ya hizo fedha
taslimu zikiwa ni shilingi 7,466, 500 na ahadi shilingi 34, 060,000/=
pamoja na vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwemo mifuko 60 ya saruji, nondo
tani moja, mchanga lori kubwa nne na kokoto tripu mbili.
MWISHO
No comments:
Post a Comment