Taasisi
inayojihusisha na kutoa ruzuku kwa asasi za kiraia hapa nchini ya Foundation
for Civil Society mapema jana imeendesha zoezi maalum la kujitolea damu kwa
ajili ya kuwasaidia wagonjwa mbalimbali wenye uhitaji wa damu katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha MOI.
Akizungumza na
waandishi wa habari mapema jana katika
zoezi hilo la uchangiaji wa damu Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil
Society Bw. Francis Kiwanga amesema kuwa, wao wameamua kuchangia damu kwa
wagonjwa ikiwa ni kama njia moja wapo ya kurudisha kitu kwa jamii.
Aidha Mkurugenzi
huyo aliendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuchangia damu nakuwataka
wajitokeze kwa wingi katika zoezi hilo
hasa vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.
“Tumekuja
hapa kuchangia damu kwa kuwa ni hospitali ya Taifa na ni sehemu yenye uhitaji mkubwa
sana wa damu. Tunawaomba watanzania wengine wajitokeze kuchangia ili kuwaokoa
watanzania wenzetu lakini pia kuunga mkono jitihada za shirika la damu salama
ambalo kila kukicha wanaelezea umuhimu wa wananchi kuchangia damu ili kunusuru
maisha ya wananchi wenzetu ” Alisema Kiwanga
Ameongeza kuwa mbali na kujitoa kwao katika zoezi
la kuchangia damu lakini pia wamejipanga kwenda kuwasaidia wasichana wanaoishi
katika mazingira magumu wa kituo cha New Hope for Girls kilichopo
Kimara jijini Dar es salaam Tarehe 27/11 mwaka huu katika siku ya Jumanne ya
kutoa.
Mmoja wa wachangiaji wa damu katika Kampeni hiyo iliyoendeshwa na Taasisi ya Foundation for Civil Society, Gloria Wangeleja(Mwenye nguo ya Rangi Nyekundu) akitoa damu mapema jana katika Hospitali ya Muhimbili jijini
Dar es salaam.
KWA upande
wake Mkuu wa Kitengo cha Maabara Moi Dokta Mbuta Jakckson alisema kuwa licha ya jitihada mbalimbali
zinazofanywa na makundi ikiwamo wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali, vikundi
vya dini lakini bado changamoto hiyo haikuweza kumalizika na kusema kuwa kwa mahitaji ya kaiwada ya damu kwa
siku ni unit 70 lakini zinazopatikana ni unit 40 mpaka 50 peke yake.
Amesema hospitali
ina wataalamu wa kutosha wa kukusanya damu, watu hawana haja ya kutia shaka na
uwezo wa taasisi hiyo katika kukamilisha zoezi hilo.
“Tumekuwa tukienda
hata nje ya kituo hiki, kwa mfano tulikwenda temeke katika msikiti mmoja hivi
jina nimelisahau, lakini pia tulifika kwenye makampuni mbalimbali kuchukua
damu. Tunachohitaji ni utayari wa raia, tuko tayari wakati wote kufika mlipo
ili tuchukue damu itakayowasaidia wagonjwa” alisema.
Aliendelea
kusisitiza kuwa hapo mwanzo wagonjwa walikuwa wakichangiwa damu kutoka kwa
ndugu na jamaa zao, lakini kwa sasa hali imebadilika na wanaochangiwa na ndugu
zao ni wachache sana ukilinganisha na wasio na watu wa kuwachangia, hali inayosababisha
kuchelewa kwa huduma kutokana na kutokuwepo na damu katika benki hiyo.
Wachangiaji wakiendelea kujitolea damu.
Naye Shabani
Mwin’juma Shekihenda, Mlemavu wa macho ambaye alijitokeza katika zoezi hilo la
uchangiaji damu, ameshindwa kutimiza azma yake hiyo baada ya kupimwa na
kugundulika kuwa damu yake ni ndogo na asingeweza kuhimili kama angetolewa.
Akizungumzia tukio
hilo, Mwin’juma anasema amesononeshwa sana na kushindwa kuchangia damu kwani
aliamini chupa ya damu yake ndogo ingeweza kunusuru maisha ya kiumbe mwingine.
Amesema Licha ya
ulemavu wake lakini anauwezo wa kutembea sehemu yoyote ile, hivyo haina maana
kuwa hana wajibu wa kusaidia wengine, ameguswa na tukio hilo na kuamua kutoka
nyumbani kwakwe Buza kwa lengo la kutoa damu.
No comments:
Post a Comment