Sunday, November 25, 2018

WFP Yakubali Kuipa Nguvu Wizara ya Kilimo

Naibu Waziri wa Kilimo Ndugu Innocent Bashungwa akijadiliana na wawakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Michael Dunford na Riaz Lodhi katika ofisi za Wizara ya Kilimo jijini Dar es Salaam
Kutoka kulia: Riaz Lodhi (Mkuu wa Kitengo cha Mnyororo wa thamani WFP), Michael Dunford (Muwakilishi wa Shirika la WFP), Naibu Waziri Kilimo Mheshimiwa Innocent Bashungwa, Bi Vumilia Zikankuba na Elimpa Kiranga katika picha ya pamoja baada ya kikao 

Naibu Waziri wa Kilimo nchini Mheshimiwa Innocent Bashungwa amekutana na muwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Michael Dunford na mkuu wa usambazaji wa shirika hilo Riaz Lodhi katika ofisi za wizara hiyo jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kuboresha ushirikiano baina ya Serikali na shirika hilo.

Katika kikao hicho ndugu Michael Dunford alielezea namna WFP imekuwa ikishirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kuboresha sekta ya kilimo kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ya kuboresha lishe, kuongeza thamani ya mazao, utafiti na ubunifu katika kilimo na pia katika masoko. Alimuhakikishia Mheshimiwa Bashungwa kuwa shirika la WFP lina nia ya dhati ya kumkomboa mkulima wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya Malengo Endelevu ya Dunia (SDG) ya kutokomeza njaa ulimwengu ni kuishukuru Serikali kwa ushirikiano ambao imekuwa ikilipatia katika kutimiza majukumu yake.

Nae Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Innocent Bashungwa amemueleza muwakilishi huyo nia ya Serikali ya kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri ya mazao ndani na nje ya nchi ambapo shirika la WFP limekubali kununua tani laki moja na nusu ya mahindi toka ghala la taifa na kuahidi kununua nyingine. Pia Mheshimiwa Bashungwa alimuhakikishia kuwa serikali itaendelea kurekebisha na kuboresha baadhi ya sheria ili kurahishisha biashara ya mazao nje ya nchi. 

Katika kikao hicho pia kilihudhuriwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) Bi Vumilia L. Zikankuba  na Elimpa Kiranga (Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula)

MWISHO.

No comments:

Post a Comment