Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (mwenye kipaza sauti) akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya Buseresere wilayani Chato mkoani Geita mara baada ya kufika kijijini hapo kukagua mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu.
Na Teresia Mhagama, Geita
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amemuagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Mkoa wa Geita, Eng. Joachimu Ruweta kuhakikisha kuwa mitaa yote katika Mji mdogo wa Katoro wilayani Geita inawaka umeme ndani ya siku saba.
Alitoa maagizo hayo jana akiwa katika ziara ya kukagua mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu katika Wilaya ya Geita na Chato mkoani Geita.
Akiwa katika Mji wa Katoro, Dkt Kalemani alikagua ujenzi wa miundombinu ya umeme katika mji huo na kukuta kuna nguzo zilizosimikwa kwa muda mrefu bila wananchi kuunganishiwa umeme.
Alisema kuwa atarudi kukagua kazi ya uunganishaji umeme katika eneo hilo ndani ya Siku Saba na endapo agizo hilo halitatekelezwa, atachukua hatua za kinidhamu kwa yeyote atakayechelewesha kazi hiyo.
Aidha aliagiza kuwa wananchi hao waunganishiwe umeme kwa bei ya shilingi 27, 000 tu na siyo gharama za TANESCO zinazoanzia shilingi 177,000 na pia kuongeza nguvu kazi ya vibarua ili kazi ifanyike kwa wakati ulioagizwa.
Katika hatua nyingine, akiwa katika Kata ya Buseresere wilayani Chato alikataa kuzindua mradi wa umeme katika kijiji cha Mapinduzi, baada ya kukuta wananchi Saba tu katika Kijiji hicho ndio wameunganishiwa umeme huku kukiwa na nguzo za umeme zilizosimikwa kwa muda mrefu bila kuwa na nyaya.
Hivyo, baada ya kukagua miundombinu ya umeme katika Kijiji hicho, alimuagiza Meneja wa TANESCO wilaya ya Chato, Eng. Nyaonge Nyabinyiri kuhakikisha kuwa wananchi wengi katika kijiji hicho pamoja na cha Ibondo wanaunganishwa na umeme ifikapo tarehe Tano, Disemba mwaka huu.
Aidha aliwaagiza watendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa, wanafungua dawati la kuhudumia wateja katikati ya Mji Mdogo wa Katoro na Kata ya Buseresere ili kuwapunguzia adha wananchi ya kufuata huduma mjini Geita au Chato.
Kwa upande wa Mameneja hao, walimuahidi Waziri wa Nishati kuwa watatekeleza maagizo hayo ndani ya muda ulioagizwa ili kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma ya umeme.
No comments:
Post a Comment