Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa
Zahanati ya Nandagala wilayani Ruangwa Novemba 19, 2018. Kushoto kwake ni Mkuu
wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandirwa, kushoto ni Mganga Mkuu wa wilaya ya
Ruangwa, Dkt. Mahela Njile na kushoto ni Mganga Mfawidhi
wa Zahanati hiyo, Abubakar Abbas Rugwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na
Waganga na Wanguzi wa Zahanati ya Nandagala wilayani Ruangwa kabla ya kukagua
ujenzi wa majengo ya Zahanati hiyo Novemba 19, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsalimia mtoto
Hamza Abdulrazak aliyepelekwa na Mama yake Mzazi, Mariam
Liwena (wapili kushoto) katika Zahanati ya Nandagala wilayani
Ruangwa kwa matibabu, Novemba 19, 2018. Watatu kushoto
ni Ajira Mpoka na mwanae Naifat Arifa. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU AWATAKA WANANCHI WAJENGE MABWENI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamewataka wananchi
kwenye Kata ya Mnacho wilayani Ruangwa washirikiane kujenga mabweni katika
shule ya sekondari Mnacho ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembelea umbali
mrefu kwenda shuleni hapo.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba 19, 2018)
wakati alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni,
ambalo ujenzi wake unagharimu sh. milioni 92.4 ikiwa ni mchango uliotolewa na
wadau wa elimu.
“Bweni hili likikamilika litawapunguzia wanafunzi
kutembea umbali mrefu kuja shuleni hususani wanaoishi vijiji vya mbali kwa
sababu wataishi hapa, jambo ambalo litachangia kuongeza ufaulu wa watoto wetu.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka
wananchi waishio katika Kata hiyo na za jirani washirikiane na kuanzisha mradi
wa ujenzi wa mabweni mengine kwa kuwa hilo moja lililojengwa na wadau halitoshi
kulingana na idadi ya wanafunzi.
Amesema yeye yuko tayari kuendelea kuwaunga mkono
wananchi hao kwenye mipango yao yote ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo
katika Kata yao, lengo likiwa ni kuhakikisha mikakati ya Serikali ya kuboresha
huduma za jamii inatimia.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi hao
washirikiane na walimu kufuatilia maendeleo ya taaluma kwa watoto wao shuleni
na kujiridhisha kama wanafanya vizuri darasani na iwapo watabaini changamoto
waweze kuzitatua kwa pamoja.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa bweni hilo, Mkuu wa
shule ya sekondari Mnacho, Mwalimu David Mwakalobo amesemma ujenzi wa bweni
hilo lenye uwezo kulaza wanafunzi 80 ulianza Septemba 19, 2018 na unatarajiwa
kukamilika Januari, 2019.
“Kutokana na idadi ya wanafunzi waliopo shuleni
bweni hili litakidhi mahitaji ya kuwalaza wanafunzi wa kike tu. Tunaendelea
kuwaomba wahisani waendelee kutusaidia ili tupate bweni lingine kwa ajili ya
kuwalaza wanafunzi wa kiume.”
Mwalimu Mwakalobo amesema iwapo watafanikiwa kuwa
na mabweni ya kuwalaza wanafunzi wote 334 shuleni hapo yatawasaidia katika
kutatua changamoto ya utoro na mdondoko wa kitaaluma kwa wanafunzi kwa sababu
wengi wanatoka mbali.
Pia mradi wa ujenzi wa mabweni utasaidia walimu
kuwa karibu na wanafunzi wakati wote, hivyo kupata muda mwingi wa kuwasaidia
wanafunzi kimasomo kwa sababu watakuwa wanaishi shuleni. “Mradi huu pia
utapunguza wanafunzi wengi wa kike kupata ujauzito.”
Ameongeza kuwa uwepo wa mabweni shuleni hapo
utaongeza ari ya wanafunzi kupenda shule tofauti na hali ilivyo sasa kwa sababu
wengi wanalazimika kutembea muda mrefu kwa kuwa wanatoka vijiji vya mbali,
jambo linalowafanya wasipende shule.
No comments:
Post a Comment