Na
Zuena Msuya, Dodoma,
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani
amewataka wakandarasi wanaotekeleza Mradi ya kusambaza umeme vijijini (REA III)
kuacha visingizio vinavyochelewesha mradi huo kukamilika kwa wakati.
Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo wakati
akizungumza wakandarasi wanaotekeleza mradi huo katika mikoa ya Mwanza na
Manyara juu ya maendeleo ya utekelezaji REA III, mzunguko wa kwanza katika
Mikoa hiyo.
Katika mkutano huo, Dkt. Kalemani
aliwaeleza wakandarasi hao kuwa, wamekuwa na visingizio vingi kila wanapoulizwa
kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika maeneo yao, na wakati
mwingine visingizio hivyo havina tija.
“Wakandarasi tekelezeni mradi wa REA na
ukamilike kwa wakati kama mikataba yenu inavyoelekeza, acheni visingizio
visivyokuwa na tija katika utekelezaji wa mradi huo, kwa kuwa vinakwamisha
shughuli za maendeleo. Unakuta mkandarasi anasingizia hana nguzo au mwingine
anakwambia nyaya, lakini kiuhalisia vifaa hivyo vipo, kwakweli hii haipendezi
na hakuna atakayevumilia ", alisema Dkt. Kalemani.
Kuhusu uwashaji Umeme katika vijiji, Dkt.Kalemani
aliwataka wakandarasi wanaotekeleza mradi wa REA katika Mikoa ya Mwanza na
Manyara kuwa kuanzia ijumaa ya wiki ijayo lazima kila kijiji kuwepo na kundi la
wafanyakazi ili kuongeza ufanisi wa kazi.
Sambamba na hilo, kila mkandarasi ahakikishe kuwa anawasha Umeme
katika vijiji 3, kwa kila wiki na kwamba mameneja wanaosimamia miradi hiyo wawe
mabalozi wazuri kwa wateja na kutumia lugha zisizoudhi.
Aidha,
katika mkutano huo, Dkt Kalemani aliwaagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja
na TANESCO kuhakikisha kuwa kila mkoa unakuwa na mtaalam mwenye kuhakiki ubora
wa miundombinu kwa ajili ya utekelezaji
wa mradi wa REA, ikiwemo nguzo, transfoma, nyaya na vifaa vingine vinavyotumika
katika mradi huo.
Vilevile,
kila Mkoa uwe na vifaa vyake kwa kutathmini ubora wa miundombinu hiyo tofauti
na ilivyo sasa ambapo vifaa vya kuhakiki ubora wa miundombinu vinazunguka
kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine jambo linalochelewesha kazi ya kuhakiki ubora
wa miundombinu hiyo.
Caption
Picha 1
Waziri
wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani( katikati) akiongoza kikao cha kujadili
maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa REA III, mzunguko wa kwanza, katika mikoa
ya Mwanza na Manyara, kikao hicho kilifanyika jijini Dodoma na kuhusisha
wakandarasi wanaotekeleza mradi huo katika mikoa hiyo pamoja na watendaji wa
REA na TANESCO.
Picha 2
Wakandarasi
wanaotekeleza mradi wa REA III, mzunguko wa kwanza, katika mikoa ya Mwanza na
Manyara pamoja na watendaji wa REA na TANESCO wakimsikiliza Waziri wa Nishati,
Dkt.Medard Kalemani aliyekuwa akiongoza kikao.
Picha 3
Waziri
wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani aliyekuwa akingoza kikao hicho, kushoto ni
Kaimu Katibu mkuu wa Wizara ya Nishati, Haji Janabi.
No comments:
Post a Comment