Monday, November 12, 2018

TANI 240 ZA MAHINDI ZATAIFISHWA, ZAGAWIWA KWA YATIMA NA SHULE


Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akimkabidhi mkuu wa shule ya sekondari ya Vwawa moja ya magunia ya mahindi ikiwa ni sehemu ya tani 240 zilizogawiwa kwa shule 18 za sekondari na vituo vya watoto yatima mara baada ya kutaifishwa na TRA kwa kuingizwa nchini kinyume na taratibu.
Tani 240 za mahindi ya chakula zilizokamatwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa kuingizwa nchini kutoka nchi jirani kinyume na taratibu zimetaifishwa na serikali na kugawiwa kwa Vituo vya watoto yatima na shule 18 za sekondari Mkoani Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amekabidhiwa mahindi hayo na kufikia uamuzi wa kuyagawa mara baaada ya kujiridhisha kuwa yaliingia nchini kinyume na taratibu na sheria, yametelekezwa kwa muda wa mwaka mmoja na wamiliki wake na bado yanafaa kwa matumizi ya chakula.
“Mahindi haya kisheria nimekabidhiwa baada ya wamiliki wake kushindwa kufuata sheria na taratibu za nchi yetu, yalitoka nchi jirani na yalikuwa yanapelekwa nchi nyingine jirani, TRA wameyataifisha na nimeona tuwagawie wanafunzi wetu na vituo vya watoto yatima wapate chakula kwakuwa mahindi haya tumejiridhisha pia kuwa yanafaa kwa chakula”, ameongeza.
Meneja wa Ushuru wa Forodha wa Kituo cha mpakani cha Tunduma John Masa  amesema bidhaa zote zitakazobainika kusafirishwa kinyume cha taratibu zitataifishwa kama walivyofanya kwenye mahindi hayo baada ya kubaini kuwa yamesafirishwa kwa kukiuka sheria hivyo yamegawiwa kwa Mkoa ambao umetoa kwa wanafunzi na watoto yatima.
Nao baadhi ya wakuu wa shule za sekondari na wawakilishi wa vituo vya watoto yatima ambao wamepokea mahindi hayo ya chakula wameipongeza serikali kwa msaada wa mahindi ambao utasaidia upatikanaji wa chakula katika shule na vituo vyao.

No comments:

Post a Comment