Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua uwanja wa
michezo wa Ilulu uliopo mjini Lindi, Novemba 21, 2018. Kushoto kwake
ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akikagua magunia ya korosho yaliyohifadhiwa
kwenye ghala la kiwanda cha korosho cha BUKO cha mjini Lindi wakati
alipotembelea kiwanda hicho, Novemba 21, 2018. Kushoto ni Mkurugenzi
wa Kampuni ya Namgongo Holding iliyopewa dhamana ya kutunza ghala
hilo, Ramadhani Katau. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamewaagiza
Warajisi Wasaidizi wa Ushirika katika Mikoa yote inayolima korosho nchini
waandae semina kwa Maafisa Ushirika, viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS),
maafisa ugani na wakulima ili kuwawezesha kubaini na kupanga korosho katika
madaraja kuanzia ngazi ya vyama vya msingi.
Amesema jambo hilo
litasaidia mkulima aweze kujua korosho aliyoipeleka ina ubora gani akiwa huko
kijijini na wanapoifikisha kwenye ghala kuu wafanye kazi ya kuthibitisha , kwa
hatua hiyo itasaidia kuondoa malalamiko kuhusu madaraja
“Zoezi hili licha
ya kuthibitisha ubora itasaidia kuboresha uzalishaji kwani wakulima
wataelimishwa namna ya kuimarisha na kuboresha uzalishaji wa korosho nchini
ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya viatilifu ’’
Waziri Mkuu ameyasema hayo
leo (Jumatano, Novemba 21, 2018) wakati alipotembelea kiwanda cha korosho cha
BUKO kilichopo kwenye Manispaa ya Lindi, ambapo ameshuhudia korosho zikipimwa
ubora kwenye ghala kuu lilipo kiwandani hapo.
Ameagiza semina ifanyike
mwakani ili maafisa ushirika baada ya kupata mafunzo wawasaidie wakulima kwenye
msimu ujao watambue korosho walizopeleka kuziuza zina ubora gani.
Waziri Mkuu amesema katika
semina hiyo wakutane maafisa kilimo na maafisa ushirika ili wapate taaluma hiyo
itakayowawezesha kupima korosho na kuitenga katika madaraja na kuwaondolea
shida wakati wa mauzo.
Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Ushirika mkoa wa Lindi,
Robert Nsunza amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wataandaa semina hiyo kwa
wahusika na kuanzia hapo wakulima wakuwa wakitambua ubora wa korosho zao
kuanzia ngazi ya kijijini.
NayeMkurugenzi wa Kampuni ya Nangomba Holdings,
Ramadhan Katau ambaye ndiye mtunzaji wa ghala la korosho katika kiwanda cha
BUKO amesema ghala hilo linauwezo wa kupokea na kutunza tani 10,000 za korosho,
hadi sasa tani zilizopo ghalani hapo ni 6,370. Hali ya ukusanyaji wa korosho
inaendelea kwa kuwa sasa ndio katikati ya msimu.
No comments:
Post a Comment