Na Mathias Canal-WK, Dodoma
Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo. Katika utekelezaji wa azma hiyo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo (ASLMs) pamoja na wadau wa sekta inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme Phase Two-ASDPII).
Lengo kuu la ASDP II ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (mazao, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha na usalama wa chakula na lishe.
Hayo yamesemwa na Mgeni rasmi Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) Leo Jumatano tarehe 7 Novemba 2018 wakati akizindua mradi wa kuimarisha usalama wa chakula na biashara ya Mazao ya kilimo (Strengthening Food Security and Export Trade in Tanzania-SFSETT) katika ukumbi wa Morena Hoteli Jijini Dodoma.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mkurugenzi wa Kanda wa Alliance for Green Revolution in Africa - AGRA – Profesa Nuhu Hatibu, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Economic and Social Research Foundation – ESRF – Dkt. Tausi Kida, Washirika wa Maendeleo – FAO; WFP, Word Bank, Wakuu wa Taasisi za Umma, Wawakilishi wa sekta binafsi, vyama vya wakulima, taasisi za utafiti, Mashirika yasio ya kiserikali (NGOs), na Asasi za kiraia.
Dkt Tizeba alisema kuwa mradi huo utawezesha kufuatilia masoko ya mazao pamoja na hali ya chakula nchini na nchi jirani na hivyo kuihakikishia serikali kuwa na Sera zinazotabirika kuhusu biashara ya mazao ya kilimo kwa kuwa sasa kutakuwa na mfumo unaotuwezesha kuwa na ushahidi (Policy evidence) katika kutekeleza Sera.
Dkt Tizeba aliwahakikishia washiriki kuwa upatikanaji wa chakula umeendelea kuwa imara kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo na hivyo wakulima na wafanyabiashara wanaosafirisha mazao ya chakula nje ya nchi likiwemo zao la mahindi na mchele waendelee kufanya hivyo kwa kufuata taratibu za biashara ya mazao zilizopo kisheria. "Serikali imedhamiria kuboresha upatikanaji wa masoko ya mazao ya chakula ili kuwawezesha wakulima kuuza mazao yao na kujipatia kipato" Alikaririwa
Amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2017/2018 na 2018/2019 Wizara ilifanya maboresho ya kisera, kisheria na kanuni mbalimbali ili kuweka mazingira wezeshi ya uendeshaji na uwekezaji katika kilimo. Katika jitihada hizo Wizara ilifuta tozo 78 kati ya 139 zilizokuwa hazina tija kwa wakulima.
Aidha, Katika mwaka 2018/2019, Wizara imefuta ada na tozo 20 ambazo kwa mwaka 2017/18 zimeonekana ama kuwa kero kwa wakulima au vikwazo kwa maendeleo ya sekta ya kilimo.
Waziri Tizeba amezitaja juhudi zingine kuwa ni pamoja na Serikali kuendelea kuimarisha mifumo mbalimbali ya masoko ikiwemo kuimarisha Ushirika ambapo mazao ya kimkakati ambayo ni Korosho, Tumbaku, Kahawa, Chai na Pamba yatatumia mfumo huo.
Katika kuhakikisha wananchi hawakopwi mazao yao, Wizara imeendelea kuhamasisha uundwaji wa Vyama vya msingi vya ushirika wa Mazao na masoko (Agricultural Marketing Cooperative Sociteies – AMCOS) ambapo juhuhudi hizo za Wizara zimeongeza idadi ya vyama kutoka 7,888 vilivyokuwepo Machi, 2015 ambapo hadi mwaka jana kufikia Disemba 2017 idadi ya vyama ilifikia 10,990 ongezeko la karibu asilimia 40.
Aidha, alisema kuwa Wizara ya kilimo inahimiza ukusanyaji na uuzaji wa mazao makuu ya biashara kupitia Vyama vya Ushirika. Utaratibu huu umesaidia katika kuongeza kiasi cha makusanyo ya mazao kupitia Vyama vya Ushirika, uhakika wa soko na kuimarika kwa bei za mazao kupitia minada.
Vilevile, mfumo wa stakabadhi ghalani na ujenzi wa maghala umeimarishwa kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanauza mazao yao kwa pamoja.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof Elisante Ole Gabriel alisema kuwa Utekelezaji wa ASDP II ni kuhakikisha kuwa Taifa linaendelea kujitosheleza kwa chakula; kuimarisha uchumi; kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda; na kuongeza ajira. Ili kufikia malengo haya; Utekelezaji wa ASDP II utazingatia mnyororo wa thamani wa mazao ya kipaumbele ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Aliongeza kuwa katika kipindi kirefu kumekuwa na changamoto za upatikanaji wa taarifa sahihi za uzalishaji wa mazao ya kilimo, masoko pamoja na mahitaji ya chakula ya ndani ya nafaka na mazao yasiyo ya nafaka hivyo mradi huo utakuwa mkombozi.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment