Mkuu wa mkoa wa Rukwa
Mh. Joachim Wangabo ametaka kupewa mpango kazi wa ujenzi unaoendelea wa Chuo
cha Ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa, kinachojengwa katika mtaa wa Kaswepepe, kata
ya Sumbawanga asilia, Wilayani Sumbawanga ili kufuatilia kwa ukaribu na kuweza
kukosoa pale mkandarasi atakapokwenda kinyume na alichokiandaa.
Amesema kuwa kwa kufanya
hivyo, itasaidia kukosoa maendeleo ya ujenzi mapema kabla mambo hayajaharibika
na si kulalamika baada ya kukamilika kwa ujenzi na kulaumu ubadhirifu
uliojitokeza wakati fursa ya kufuatilia ilikuwepo.
“Ningependa nipatiwe
“Work plan” mpango kazi ambao mnao, hatua kwa hatua ili na mimi nikikaa kule
najua mwezi lazima mko hatua Fulani, nikiona inafaa ntakuja kukagua, mwenyekiti
wa ulinzi na usalama Wilaya nae apewe mpango kazi, Mstahiki Meya nae apewe ili
tufuatilie kwa pamoja ili kama kuna mapungufu tuambiane mapema, tusingoje
kuviziana kwamba hili limeharibika,” Alisisitiza.
Ameongeza kuwa kwenda
vibaya kwa mambo na kufika mwisho itashindikana kurudisha nyuma na matokeo yake
ni kumfunga mhusika aliyesababisha uharibifu wakati fedha za serikali
zimekwishapotea na huku wananchi bado wanahitaji maendeleo. Ameyasema hayo
alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa chuo hicho.
Kwa upande wake akisoma
taarifa ya ujenzi Mkadiriaji majengo wa ujenzi huo Faraji Selemani alisema kuwa
ujenzi huo utagharimu shilingi bilioni 10.7 hadi kukamilika kwake ambapo
kutakuwa na majengo tisa yatakayohusisha fani mbalimbali pamoja na jengo la
utawala.
“mradi utakuwa na
majengo yafuatayo, majengo ya utawala, madarasa pamoja na maktaba, “workshops”
mbali mbali 9, mabweni ya wanafunzi wa kike na wakiume, vyumba vya waalimu na
makazi yao na sehemu ya kufanyia mazoezi kwa vitendo,” Alimalizia.
Ujenzi huo ambao umeanza
mapema mwezi wa tisa mwaka huu baada ya makabidhiano baina ya VETA makao makuu
Dar es Salaam, VETA kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya pamoja na Ofisi ya mkuu
wa mkoa wa Rukwa kumkabidhi mkandarasi TENDER Intarnational kwaajili ya ujenzi
wa chuo hicho huku mshauri elekezi akiwa Sky Architect Consultancy Ltd.
Ujenzi ukikamilika chuo
kitaweza kuchukua wanafunzi 900 wa kozi ndefu na 600 wa kozi fupi hivyo,
kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1,500.
No comments:
Post a Comment