Saturday, October 13, 2018

DKT TIZEBA AWATAKA WAKULIMA WA PARETO KUJIUNGA NA MFUMO WA USHIRIKA

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na wakulima wa Pareto katika kijiji cha Ikanga kilichopo kata ya Mdabulo Wilayani Mufindi kwenye mkutano wa hadhara akiwa katika muendelezo wa ziara ya kikazi Mkoani Iringa, Jana tarehe 13 Octoba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, WK)
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akikagua shamba la Pareto la mkulima Bahati Mhapa, katika kijiji cha Ikanga Wilayani Mufindi kwenye mkutano wa hadhara akiwa katika muendelezo wa ziara ya kikazi Mkoani Iringa, Jana tarehe 13 Octoba 2018. 
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akizungumza na wakulima wa Pareto katika kijiji cha Ikanga kilichopo kata ya Mdabulo Wilayani Mufindi kwenye mkutano wa hadhara akiwa katika muendelezo wa ziara ya kikazi Mkoani Iringa, Jana tarehe 13 Octoba 2018. 
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akikagua kiwanda cha Pareto Mafinga (PCT) kilichopo mamlaka ya Mji wa Mafinga wakati akiwa katika muendelezo wa ziara ya kikazi Mkoani Iringa, Jana tarehe 13 Octoba 2018. 

Na Mathias Canal-WK, Mufindi-Iringa

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) amewataka wakulima wa Pareto kote nchini kujiunga na mfumo rasmi wa vyama vya msingi vya ushirika.

Dkt Tizeba ametoa Mwito huo Jana tarehe 13 Octoba 2018 wakati akizungumza na wakulima wa Pareto katika kijiji cha Ikanga kilichopo kata ya Mdabulo Wilayani Mufindi kwenye mkutano wa hadhara akiwa katika muendelezo wa ziara ya kikazi Mkoani Iringa.

Alisema kuwa ushirika ni dhana ya kuleta maendeleo kwa kushirikiana ambapo dhana hiyo imefanikiwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita.

“Kutokana na changamoto mbalimbali zilizoikumba sekta hii ya ushirika watu wengi wamekosa imani na vyama hivi na baadhi ya vyama vimeshindwa kufanya kazi vizuri hivyo nawahakikishia serikali inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli imerejesha nidhamu kwenye ushirika” Alikaririwa Dkt Tizeba na kuongeza kuwa

Alisema kuwa Ushirika maana yake ni muungano wa watu ambao wanafanya kazi pamoja kwa hiari ili kufanikisha mahitaji yao ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kupitia shughuli ya biashara inayomilikiwa kwa pamoja na kudhibitiwa kidemokrasia. Ushirika unazingatia maadili ya kujisaidia wenyewe, jukumu binafsi, demokrasia, usawa na mshikamano.

Wanachama wa Ushirika wanaamini katika misingi ya uaminifu, uwazi, uwajibikaji kwa jamii na kuwajali wengine. Muundo wa Ushirika kwa ujumla unategemea uimara wa chama cha msingi cha Ushirika, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha vyama imara vya msingi vinaanzishwa.

Wakulima wa Pareto katika Mikoa ya Nyanda za juu Kusini na maeneo yote nchini wanapaswa kulima kwa wingi zao hilo ili waweze kuinua kipato chao na kuondokana na umaskini kutokana na kuwepo kwa uhakika wa soko la zao hilo.

Aidha, Waziri Tizeba amesimamisha utendaji kazi wa Wakala wa ununuzi wa Pareto Wilayani Mufindi Ndg Nilbet Kabonge badala yake amemtaka mwenyekiti wa kijiji kuitisha mkutano wa kijiji ili kuchagua wakala mwingine atakayesimamia maslahi ya wakulima.

“ Tena Mkurugenzi wa Halmashauri unapaswa kuhakikisha kuwa unanunua mzani maalumu kwa ajili ya kupima ubora wa zao la Pareto kwani kufanya hivyo kutaondoa udanganyifu wa muda mrefu kwenye zao hili” Alisema

Kadhalika, aliutaka uongozi wa Wilaya ya Mufindi na uongozi wa Mkoa wa Iringa kusimamia ipasavyo upimaji wa ubora wa zao la Pareto ili kuepusha wizi na udanganyifu kwa wakulima wanaouza Pareto yao kupitia mawakala wenye vipimo ambavyo havijathibitishwa na wakala wa vipimo nchini.

Pareto ni  moja kati ya zao ambalo hulimwa Tanzania, na huwa ni zao jamii ya ua ambalo hutumika kutengenezea dawa za kuuwa wadudu shambani (insecticide) hujulikana kama pyrethtin.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment