Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga
akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ng’arika Kata ya Sapiwi Septemba
14, 2018 wilayani humo, katika Uzinduzi wa zoezi la uthamini na upimaji
wa maeneo ambayo Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Simiyu kitakapojengwa
.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji
cha Ng’arita katika Kata ya Sapiwi Wilaya ya Bariadi, wakinyoosha mikono yao
juu kumhakikishia Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Festo Kiswaga kuonesha utayari wao
wa kuachia maeneo yao kupisha Ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha
mkoa huo, wakati wa Mkutano wa kufungua Zoezi la tathmini na upimaji wa
maeneo hayo, Septemba 14, 2018.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Wananchi wa Vijiji vya Igegu na Nga’arita Kata ya Sapiwi
wilayani Bariadi wameridhia kuachia maeneo yao kupisha Ujenzi wa Kiwanja
cha Ndege cha Kimataifa Mkoani Simiyu ambacho kinatarajiwa kujengwa katika eneo
la Igegu wilayani .
Wananchi hao wameyasema hayo Septemba 14, 2018 wakati wa
uzinduzi wa zoezi la Uthamini na upimaji wa maeneo hayo, ambalo linatarajiwa
kumalizika baada ya mwezi mmoja na wiki mbili kuanzia sasa.
Wamesema kuwa wamefurahishwa na hatua ya Serikali kujenga
Kiwanja cha Ndege wilayani Bariadi na kwa kuwa ujenzi huo ni suala la maendeleo
hawawezi kupinga, huku wakiiomba Serikali kuhakikisha wanalipa fedha za fidia
kwa wakati mara tu baada ya kukamilisha zoezi la uthamini na upimaji wa maeneo
hayo.
“Kwa kuwa ujenzi wa kiwanja cha ndege ni maendeleo hatuwezi
kukataa kutoa maeneo yetu, tumekubali kutoa maeneo ila ombi letu kwa Serikali
tunaomba tulipwe fidia ya maeneo yetu kwa wakati na tulipwe kwa haki” alisema
Ndaturu Malemi mkazi wa Kijiji cha Igegu.
“Tumekubali kutoa maeneo yetu Uwanja wa Ndege ujengwe, ushauri
wangu tu ni kwamba kwa kuwa tunaelekea msimu wa kuandaa mashamba baada ya
tathmini tunaomba tuliokuwa na maeneo hapa tuambiwe mapema kama ujenzi utaanza
au tunaweza kuendelea na shughuli za kilimo”alisema Mahembe Mayumba mkazi
wa Kijiji cha Igegu
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga
amewataka Wataalam wa Ardhi watakaohusika na zoezi la uthamini na upimaji
wa eneo litakojengwa Kiwanja hicho cha Ndege kufanya zoezi hilo kwa kufuata
haki na sheria za nchi.
“Nimewaagiza wataalam watakaohusika kufanya zoezi la tathmini na
kulipa fidia kwa kumuogopa Mungu, watende haki, kila ambacho mwananchi anapaswa
kufidiwa wahakikishe kinafidiwa kwa mujibu wa sheria; tumekubaliana wataalam
watavaa vitambulisho ili watambuliwe na ikitokea mtu akihujumu zoezi hili iwe
rahisi kumfahamu na kuchukua hatua” alisema Kiswaga.
Akizungumzia suala la taarifa ya uthamini kutolewa mapema
kwa wananchi, Kiswaga amesema kuwa zoezi hilo litafanyika kwa muda wa mwezi
mmoja na wiki mbili na baada ya hapo wenye maeneo watapewa taarifa.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga Bi.Beaster Dotto
Madale amesema Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa utawasaidia wananchi
kupata usafiri wa anga ambao ni wa haraka, uhakika na salama, huku akisisitiza
kuwa kiwanja hicho kitakapoanza kujengwa wananchi hususani vijana watapata
ajira kwenye kazi za ujenzi na wanawake watajiajiri katika kazi za kupika na
kuuza vyakula
Naye Afisa Ardhi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Bi.
Bi. Cecilia Mwing’uri amesema Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Nchini
(TAA) imeshatoa fedha kwa ajili ya tathmini, uthamini na upimaji wa maeneo
Kiwanja kitakapojengwa na mara baada ya zoezi hilo kukamilika wananchi
wanaohusika watalipwa fidia.
Bi.Cecilia
amewahakikishia wananchi wa Vijiji vya Igegu na Ng’arita kuwa watalipwa fedha
zao zote mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki , kwa kuwa Mamlaka
ya Viwanja Vya Ndege Nchini (TAA) imetenga fedha hizo kwa ajili ya fidia ya
Kiwanja cha Ndege cha Simiyu.
Kwa mujibu wa Meneja
wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga Bi.Beaster Dotto Madale Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa Mkoani Simiyu kitakapokamilika kitakuwa ni miongoni mwa Viwanja
vikubwa hapa nchini ambavyo vina uwezo wa kupokea ndege kubwa.
MWISHO
No comments:
Post a Comment