Monday, September 3, 2018

DKT TIZEBA ASHIRIKI HAFLA YA UTIAJI SAINI MKATABA WA UJENZI WA MELI MPYA NA CHELEZO KATIKA ZIWA VICTORIA

Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Dkt Charles Tizeba ambaye ni Waziri wa kilimo (Kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Ndg Kheri James mara baada ya kushiriki hafla ya utiaji saini mikataba minne (4) katika eneo la Mwanza South Jijini Mwanza ambapo mgeni rasmi alikuwa Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, leo tarehe 3 Sepetemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, WK)Wananchi wakishuhudia tukio la utiaji saini mikataba ya ujenzi wa melMhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na mawaziri wa sekta ya kilimo, Viwanda na biashara, Ardhi nyumba na Maendeleo ya makazi, wakuu wa mikoa ya Mara, Mwanza na Geita muda mchache baada ya kushiriki hafla ya utiaji saini mikataba minne (4), leo tarehe 3 Sepetemba 2018.
Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba (kulia) akiteta jambo na Waziri wa biashara, viwanda na uwekezaji Mhe Charles Mwijagewakiwa katika hafla ya utiaji saini mikataba minne (4) katika eneo la Mwanza South Jijini Mwanza ambapo mgeni rasmi alikuwa Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, leo tarehe 3 Sepetemba 2018.

Mathias Canal, WK-Mwanza

Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Dkt Charles Tizeba ambaye ni Waziri wa kilimo leo Jumatatu tarehe 3 Sepetemba 2018 ameshiriki hafla ya utiaji saini mikataba minne (4) ambapo Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ndiye alikuwa Mgeni rasmi katika kushuhudia tukio hilo.

Uwekaji saini wa mikataba hiyo minne umefanyika baina ya kampuni ya huduma za meli (MSCL) na makampuni kutoka Jamhuri ya watu wa Korea kusini ambapo mikataba hiyo imehusisha ujenzi wa meli moja mpya, ujenzi wa chelezo ya kujenga meli hiyo, ukarabati wa meli ya MV Victoria na ukarabati wa meli ya MV Butiama.

Akizungumza katika hafla hiyo Rais Magufuli amewataka wakandarasi hao kufanya kazi kwa weledi na kumaliza haraka ujenzi wa meli hiyo ili kuongeza ufanisi ya tija kwa wananchi hususani katika mikoa ya Kagera na Mwanza.

Alisema kuwa tukio hilo la utiaji saini ni hatua ya awali ya kuanza rasmi utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo ujenzi wa meli kubwa na ya kisasa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi inayohusu uboreshaji wa usafiri majini katika ukanda wa ziwa Victoria na nchi jirani.

Mhe Rais aliongeza kuwa meli mpya pindi itakapokamilika itakuwa meli kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Tanzania na itaongoza kwa ukubwa kuliko meli zote zilizopo katika maziwa makuu.

Meli hiyo kubwa na ya kisasa itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo pamoja na magari madogo 20 kwani itakapomalizika ujenzi wake na kuanza kutoa huduma itasaidia kurahisisha usafiri katika mwambao wa ziwa Victoria kwa kutoa huduma ya uhakika, haraka na salama kwa kutumia gharama nafuu.

Meli hiyo inatarajiwa kufanya safari zake kati ya Mwanza na Bukoba kupitia bandari ya Kemondo, Mwanza na Musoma na pia kati ya Mwanza na bandari ya nchi jirani za Kenya na Uganda ambapo kufanya hivyo itasaidia kusaidia ufanyaji wa biashara na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi kwa ujumla katika mikoa ya Kanda ya ziwa.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele kumthibitisha Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya huduma za meli (MSCL) Ndg Eric B. Hamissi kuwa Meneja Mkuu kutokana na utendaji wake uliotukuka ili aweze kuongeza tija katika utendaji kazi.

Mikataba mingine iliyosainiwa katika hafla hiyo ni wa ukarabati mkubwa wa meli ya MV Victoria yenye uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 200 za mizigo sambamba na mkataba wa ukarabati wa meli ya MV Butiama yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 za mizigo.

MWISHO

No comments:

Post a Comment