Thursday, August 30, 2018

DKT TIZEBA AMUHAKIKISHIA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA KUKAMILISHWA VYUMBA 10 VYA MADARASA SHULE YA SEKONDARI KASISA

Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mkoani Mwanza ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba akitoa salamu za wananchi wa Jimbo hilo kwenye sherehe za Mwenge wa Uhuru katika kata ya Kasisa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Mkoani Mwanza, Leo tarehe 30 Agosti 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo)
Muonekano wa mradi wa kisima kirefu cha maji Kasisa mara baada ya uzinduzi wa mradi huo wakati wa sherehe za mbio za Mwenge kitaifa katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Leo tarehe 30 Agosti 2018.
Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mkoani Mwanza ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba akikabidhiwa Mwenge wa uhuru ili kuulaki wakati wa mapokezi ya sherehe za Mwenge wa Uhuru katika eneo uwanja wa michezo Isenyi Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Mkoani Mwanza Leo tarehe 30 Agosti 2018. 

Muonekano wa zahanati ya Kafunzo mara baada ya kuzinduliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Mhandisi Charles Kabeho Leo tarehe 30 Agosti 2018.
Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mkoani Mwanza ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba akipanda mti mara baada ya kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Kasisa wakati wa sherehe za Mwenge wa Uhuru katika kata ya Kasisa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Mkoani Mwanza Leo tarehe 30 Agosti 2018

Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mkoani Mwanza ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba akizungumza kwenye sherehe za Mwenge wa Uhuru katika shule ya sekondari Iligamba kata ya Iligamba iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Mkoani Mwanza Leo tarehe 30 Agosti 2018

Na Mathias Canal, WK-Mwanza

Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mkoani Mwanza ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba amemuhakikishia kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Ndg Charles Kabeho kufikia mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu 2018 mradi wa ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa ya shule ya Sekondari Kasisa utakuwa umekamilika.

Waziri Tizeba ametoa kauli hiyo leo tarehe 30 Agosti 2018 katika kata ya Kasisa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa wakati akitoa salamu za wananchi wa Jimbo hilo kwenye sherehe za Mwenge wa Uhuru ambao umeingia katika Halmashauri ya 149 tangu ulipowashwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa Mkoani Geita mwezi Aprili mwaka huu.

Dkt Tizeba alisema kuwa kukamilika kwa vyumba hivyo vya madarasa kutarahisisha huduma za upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi katika kata hiyo kwani umbali wanaotumia kwenda shuleni katika kipindi kirefu umekuwa ukififihisha juhudi za ufaulu kutokana na umbali mrefu wanaotumia wanafunzi hao kufika shuleni.

Alisema kuwa mpango wa serikali ya awamu ya tano inayokngozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kuboresha huduma za elimu nchini ili kuwa na Taifa endelevu kifikra na weledi katika utendaji jambo litakaloongeza chachu katika uzalishaji na tija kwa maendeleo ya wananchi.

Katika hatua nyingine Dkt Tizeba amempongeza kiongozi huyo wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa kukubali na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa madarasa ya sekondari Kasisa, Kuzindua mradi wa kisima kirefu cha maji Kasisa, Kutembelea mradi wa kuongeza thamani ya mazao  Irenza sambamba na kukabidhi vyandarua kwa kinamama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano mara baada ya uzinduzi wa wa Zahanati ya Kafunzo.

Alisema kuwa kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa uhuru kwa mwaka huu 2018 inasema “Elimu ni ufunguo wa maisha; Wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu” Kauli mbiu hiyo inahamasisha na kuwataka wazazi kuongeza tija katika usimamizi wa elimu kwa watoto wao huku ikiwataka watendaji wa serikali kusimamia matakwa na maelekezo ya serikali ili kuongeza ufanisi katika elimu.

Naye kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Mhandisi Charles Kabeho akizungumza kwa nyakati tofauti amempongeza Mbunge wa Jimbo la Buchosa ambaye ni Waziri wa kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba kwa ushirikiano mzuri na wananchi katika jimbo lake jambo linalopelekea kuongeza tija katika utendaji na kuzidisha chachu ya maendeleo kwa wananchi.

Alisema kuwa wananchi wanapaswa kuongeza ushirikiano kwa viongozi wao wa serikali ili kuongeza chachu ya maendeleo hususani katika sekta ya elimu kwani serikali imewekeza katika rasilimali elimu ambapo imefuta malipo ya ada kwa wanafunzi hivyo wanafunzi wote kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari kunufaika na elimu bila malipo.

Aliwasisitiza wazazi kote nchini kuongeza kasi ya usimamizi wa watoto wao na kufuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto hao kwani kumuachia mwalimu pekee jukumu la malezi kwa wanafunzi haitoshelezi badala yake kwa ushirikiano wa pamoja kati ya mwalimu, mzazi na serikali.

Alisema kuwa zipo sekondari ambazo bado hazijakamilisha ujenzi wa maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi likiwemo somo la Fizikia, Bailojia pamoja na Kemia jambo ambalo linapunguza ufanisi na tija ya kuwa na wataalamu wengi katika fani hizo hivyo wakurugenzi kote nchini wanapaswa kusimamia maelekezo ya serikali ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa maabara. 

Mwenge wa Uhuru unaendelea kutunza huistoria na falsafa ya ukombozi wa taifa, kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuendelea kuenzi amani, mshikamano, upendo na zaidi kupambana na aina yoyote ya kuwabagua watanzania kwa rangi, dini au makabila yao.

MWISHO

No comments:

Post a Comment