Thursday, August 2, 2018

MBUNGE WA JIMBO LA MANONGA, MH. GULAMALI AKUTANA NA SERIKALI YA WANAFUNZI CHUO CHA USAFIRISHAJI




Na Francis Daudi

Mbunge wa jimbo la Manonga Mh. Seif Khamis Gulamali amekutana na Uongozi wa serikali ya wanafunzi chuo cha Usafirishaji(NIT) katika dhifa fupi iliyoandaliwa chuoni hapo.

Mh. Gulamali ambaye ni kati ya wabunge vijana na walioweza kutekeleza ahadi zao za uchaguzi kwa zaidi ya asilimia tisini katika majimbo yao alipokelewa na baraza la mawaziri katika chuo.

Akieleza historia yake ya Uongozi huku akipigiwa makofi na kushangiliwa muda wote, Mh. Gulamali alitilia mkazo kuwa wanafunzi hao ili waweze kufika mbali wanahitaji kuwa wenye Nidhamu, Wavumilivu, Wabunifu na wenye uadilifu bila mawaa ya aina yoyote.

Mh. Gulamali ambaye amepata kuwa raisi wa serikali ya wanafunzi chuo cha Usafirishaji(SONIT) kati ya 2010 na 2011 alieleza kuwa wakati Fulani ilimpasa kutoa fedha zake binafsi alizotumiwa na wazazi kulipia baadhi ya wanafunzi chuoni waliozuiliwa kufanya mitihani.

Aliongeza kuwa alipata kuingia matatani kwa kutoa michango ya wanafunzi kulipia wanafunzi toka familia masikini. Nyakati zote alisimama na wanyonge hasa wanafunzi ambao walikuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali.

Kutokana na siasa za chuoni, mara kadhaa alikwazana na uongozi wa chuo akipigania haki za wanafunzi. Harakati zake zilipelekea mgomo mkubwa wa wanafunzi chuoni hapo uliofanikiwa kupaza sauti na serikali ilitatua matatizo kama vile kutokuwepo kwa mtandao wa intanet(WI-FI), jenereta kubwa, Matanki ya maji na kukosekana kwa mkuu wa chuo wa kudumu kwa miaka mingi.

Wiki moja baada ya kumaliza mitihani ya mwaka wa tatu, Gulamali aliomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga 2011. Alishika nafasi ya sita kati ya watia nia 14. Hakukata tamaa, aliungana na Dkt. Dalali Peter Kafumu ambaye alishinda ubunge kwa tiketi ya CCM.

Baadae 2012 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa jumuia ya vijana(UVCCM) kwenye mkoa wa Tabora. Nafasi zote hizo alizitumikia kwa uaminifu na uadilifu mkubwa hivyo aliheshimika mno, anasisitiza

‘Kuna kipindi unapimwa, hivyo kama una tamaa unaweza haribu kabisa malengo yako! Mfano tu, mimi kuna watu walikuwa wakinituma kufanya kazi, au hata kukukabidhi kiwango Fulani cha fedha ili kujua uaminifu. Unapewa milioni moja mara zingine tano na hata milioni mia moja, Na sikuchukua hata shilingi mia moja’

Gulamali alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo jipya la Manonga mwaka 2015, katika miaka mitatu ameweza kukifufua kiwanda cha Manonga Gunnery kilichofungwa Zaidi ya miaka 20 iliyopita, Ametoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wote waliochaguliwa kidato cha tano na sita toka katika jimbo la Manonga. 

Haitoshi amewezesha ujenzi wa mabweni na madarasa ya gharama ya zaidi ya milioni 265 na hivyo jimbo hilo litakuwa na shule tatu za kwanza tangu nchi ipate uhuru zitakazopokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Vijiji vyote 56 katika jimbo la Manonga vitaunganishwa umeme mwaka huu wa fedha 2018/19. Pia Mh. Gulamali amekamilisha kituo cha Afya Simbo kilichogharimu Zaidi ya milioni 400 ambacho kinaondoa usumbufu wa wananchi kutembea umbali mrefu kupata huduma za Afya.

Akihitimisha hotuba yake, aliwasisitizia Viongozi wa serikali ya wanafunzi chuo cha Usafirishaji(SONIT) kuweka mbele masomo na nidhamu wakati wote. Pia Mh.Gulamali ameahidi kutoa vifaa vya michezo kama vile jezi na mipira kwa timu za chuo hiko kama alivyofanya kwa miaka yote tangu awe mbunge miaka mitatu iliyopita.



Mwisho!

No comments:

Post a Comment