Na Asteria Muhozya,
Simanjiro
Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema kuanzia sasa
Serikali itaanza kutoa Leseni za madini biashara ya madini kwa masharti magumu
huku ikimtaka kila mwombaji kutoa taarifa
za mauzo ya uzalishaji, usafirishaji pamoja na mnyororo mzima wa biashara ya
madini ikiwemo fedha zinazoingia nchini kutokana na biashara hiyo.
Pia, ameiagiza Tume ya Madini kuchukua hatua stahiki kwa
kuhakikisha kila jambo katika mnyororo huo linasimamiwa kikamilifu na kuongeza
kuwa, yeye kama waziri mwenye dhamana atahakikisha anafuatilia kila hatua
itakayochukuliwa na tume hiyo.
“Tume ichukue hatua. Nitakuwa na ninyi. Msiache hata mmoja
atakayekwenda kinyume na haya. Nilifanya hivyo katika Sekta ya Utumishi wa Umma
hata huku kwenye sekta ya madini, sitashindwa kufanya hivyo,” alisisitiza
Waziri Kairuki.
Waziri kairuki aliyasema hayo jana tarehe 3 Agosti, Wilayani
Simanjiro Mkoa wa Manyara wakati akipokea taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa
kuchunguza mnyororo wa madini ya vito nchini.
Kamati hiyo ilifanya kazi yake kwa muda wa siku 30 kuanzia tarehe 26 Aprili, 2018 kwa jukumu la kuchunguza mnyororo wa madini ya vito kuanzia kuzalisha hadi usafirishaji nje ya
nchi pamoja na kubaini sababu za utoroshaji wa madini na kupendekeza hatua za
kuchukuliwa ili kuzuia utoroshaji.
Pia, aliiagiza tume ya madini kuanzia tarehe 4 Agosti,
kuhakikisha inapata taarifa za uzalishaji za migodi yote inayozalisha huku
akitaka migodi husika ieleze mahali inakouzia madini yao, anayeuziwa madini
hayo na kuongeza kuwa, zoezi husika linawajumuisha pia dealers.
Waziri Kairuki alisema, wizara yake imeamua kusimamia suala
husika ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli za kuhakikisha kuwa rasilimali
madini zinawanufaisha watanzania wote.
“ Lazima watanzania tutambue kuwa madini haya yanamilikiwa na
watanzania wote. Tunatakiwa kuyalinda kwa ajii ya maendeleo yetu na kwa manufaa
ya vizazi vijavyo,” alisema Kairuki.
Akizungumzia biashara ya madini ya tanzanite katika ukuta
unaozunguka migodi ya tanzanite mirerani, alisema hakuna serikali inayotaka
watu wake wasifanye biashara, hivyo, lengo la ukuta huo ni kuhakikisha kwamba
inadhibiti utoroshaji wa madini na kuweka mfumo mzuri ambao utawezesha madini
hayo kuzinufaisha pande zote.
Alisema tayari wizara imeandaa Kanuni za Mirerani (Mirerani
Contolled Area) ambazo hivi sasa zinafanyiwa maboresho baada ya kuwepo changamoto kadhaa katika
utekelezaji wake.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alisema serikali
imebaini baadhi ya wenye leseni za
‘broker’ kukaribisha wageni kutoka nje kufanya biashara hiyo kinyume na
taratibu na hatimaye kusafirisha madini
hayo, hivyo, aliwataka wote wanaofanya hivyo kuacha mara moja na kuwataka
watanzania wote wenye taarifa kuhusu suala hilo kutoa taarifa katika mamlaka zinazohusika.
“Kamati hii imefanya uzalendo na imefanya kazi kubwa sana.
Nimeipokea taarifa ya kamati lakini natamani wangenitajia majina ya
watoroshaji. Nilitamani sana kuona majina lakini naamini itaniuma sikio,”
alisisitiza Waziri Kairuki.
Pia, aliongeza kuwa serikali itazifuta leseni za uchimbaji madini kwa wale wote ambao
wameshindwa kuyaendeleza maeneo yao na kupewa wengine wenye nia ya dhati ya
kuendeleza shughuli za uchimbaji madini nchini.
Akizungumzia mkakati wa serikali katika kuhamasisha shughuli
za uongezaji thamani nchini, alisema kuwa serikali inaendelea kukiimarisha
kituo cha TGC kilichopo jijini Arusha, kwa kuongeza wataalam katika masuala ya
ukataji na unga’rishaji wa madini ya vito.
“Tayari tumepata walimu
7 kutoka nchini India, lakini bado tunafuatilia wengine kutoka nchini
Thailand,”alisema Kairuki.
Akiwasilisha taarifa
ya Kamati kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mratibu wa Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC),
Eric Mpesa alisema Kamati husika ilipata fursa ya kutembelea mgodi wa Mundarara
mpaka wa Namanga, Uwanja wa ndege wa KIA, Machimbo ya Tanzanite Mirerani, TGC,
Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Morogoro na Machimbo ya Epanko, Morogoro.
Akiwasilisha mapendekezo ya kamati husika Mpesa alisema kuwa,
kamati inapendekeza Serikali kutengeneza mpango wa makazi katika eneo
lililozungushiwa ukuta wa Mirerani ikizingatia uwepo wa eneo la uchimbaji,
biashara, uanzishwaji wa kituo cha One
Stop Centre, huduma za kijamii, maegesho ya vyombo vya usafiri, maeneo ya
starehe na maeneo ya utalii.
Pia, alisema serikali ihakikishe kuweka mfumo wa ulinzi
katika eneo lililozungushiwa ukuta na pia ilishauri serikali kuongeza wataalam
wa Wizara katika maeneo ya migodi ili kurahisisha ufanyaji biashara na
kuwezesha kuzuia utoroshaji wa madini ya vito.
Pendekezo lingine ni serikali kuwawezesha wachimbaji wadogo
kupata teknolojia za kisasa pamoja na tafiti za kijiolojia kufanywa na
watalaam kutoka Taasisi ya Jiolojia na
Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa malipo ya gharama nafuu yatakayolipwa baada ya uzalishaji kupatikana.
Pia, Kamati ilipendekeza seriakali kuishawishi mifuko ya
jamii isaidie wadau kuanzisha benki ya
Madini itakayowapa wachimbaji na wafanyabiashara mikopo yenye masharti nafuu.
Akizungumzia mcchango wa sekta ya madini, alisema sekta hiyo
inachangia fedha za kigeni cha kiasi cha wastani wa dola za Marekani milioni
27.8 kwa mwaka isipokuwa almasi na kati ya hizo, asilimia 27.8 ni madini
yaliyosanifiwa na kunga’rishwa na asilimia 71.3 ni madini ghafi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa
ikichazewa kwa wadau katika migodi kutokulipa kodi stahiki za serikali.
Aliishauri wizara kufuta leseni za wale wote walioohodhi
maeneo yao bila kuyafanyia kazi ili kuwezesha leseni husika kutumiwa na wengine
wenye nia ya kuendeleza sekta ya madini.
Kuhusu suala la mikataba
ya ajira katika migodi hiyo aliishauri serikali na wadau kukaa pamoja na
kujadili suala husika na kulitafutia ufumbuzi.
Kamati iliyoandaa taarifa husika ilikuwa na wajumbe 13 ikiongozwa
na Mwenyekiti Sammy Mollel, Makamu Mwenyekiti Hamis Kim, Katibu Adam Rashid
pamoja na wajumbe 10 na Sekretarieti.
Wajumbe wa Kamati hiyo walitoka TAMIDA, MAREMA, AREMA,
RUVREMA, TAWOMA, BROKER pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya Madini na TGC.
No comments:
Post a Comment