Na
Asteria Muhozya, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof.
Simon Msanjila na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT,
Mhandisi Morgan Nyonyi wamesaini Mikataba Mitatu ya kuanza ujenzi wa Vituo Saba
vya Umahiri pamoja na Jengo la Mafunzo kwa Wachimbaji wadogo katika Chuo Cha
Madini, Dodoma.
Hafla ya utiaji saini mikataba hiyo
imefanyika leo tarehe 9 Julai, 2018, Makao Makuu ya Wizara ya Madini jijini
Dodoma na kushuhudiwa na Waziri wa Madini Angellah Kairuki na Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo.
Akizungumza baada ya utiaji saini,
Waziri Kairuki amesema kuwa, tukio hilo
ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati
akiwasilisha Bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa
Mwaka wa Fedha 2018/19 ambapo alieleza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini
itaanza ujenzi wa ofisi saba za madini ili zitumike kama vituo vya umahiri
vya masuala ya madini.
Waziri Kairuki amezitaja ofisi hizo
kuwa ni Mpanda, Songea, Chunya, Tanga, bariadi, Bukoba na Musoma na kuongeza
kuwa, ni pamoja na upanuzi wa miundombinu ya Chuo Cha Madini Dodoma kwa ajili
ya kuwezesha utekelezaji wa shughuli za madini zinazotekelezwa na Chama Cha
Wachimbaji Madini Wanawake.
“ Ujenzi wa Vituo hivyo unatekelezwa
kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ambapo moja ya
malengo mahususi ya mradi huu ni kuboresha Sekta ya madini nchini hususan
kuwasaidia wachimbaji wadogo ili kuwaongezea ujuzi katika eneo la uchimbaji wa
madini na kukuza uchumi,” amesisitiza Kairuki.
Akizungumzia umuhimu wa vituo hivyo,
alisema vimelenga katika kutoa mafunzo ya jiolojia hususan katika utafiti wa
madini, mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa
mazingira hususan zisizotumia kemikali ya Zebaki.
Ameongeza kuwa, vituo hivyo pia
vitatoa mafunzo ya biashara ya madini kwa wachimbaji wadogo wa madini, mafunzo
ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo ya namna bora za utunzaji wa
mazingira kwenye migodi ya wachimbaji wadogo.
Kuhusu gharama za ujenzi wa vituo
hivyo amesema kuwa ujenzi wake utagharimu jumla ya shilingi Bilioni 11.9.
Akizungumzia sababu za kuingia Mkataba
na SUMA JKT, Waziri Kairuki amesema kuwa, jeshi hilo limekuwa likijihusisha na
kazi mbalimbali za ujenzi, kujiimarisha
kwao nchini, uwezo wao kiufundi katika kutekeleza miradi mikubwa, gharama
nafuu, ubora na kuongeza kuwa, mkataba na SUMA JKT utaokoa kiasi cha shilingi milioni 249.3 ikilinganisshwa na
wakandarasi wengine.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo,
Prof. Msanjila amesema kuwa, ujenzi wa vituo hivyo umelenga kuwasaidia wananchi
na zaidi ukilenga wachimbaji wadogo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT, Mhandisi Morgan Nyonyi amesema
kuwa, Jeshi hilo limejipanga kutekeleza mradi huo ndani ya muda uliopangwa wa
kipindi cha miezi sita na utekelezaji
wake utafanywa kwa weledi.
Kazi ya ujenzi wa vituo hivyo itasimamiwa
na washauri Elekezi Kampuni ya Y & P
Architects ambayo imesanifu majengo ya
Chuo Cha Madini Dodoma na Kampuni ya Interconsult Ltd ambayo imesanifu
majengo ya Musoma, Bariadi na Bukoba.
No comments:
Post a Comment