Monday, July 9, 2018

KUNA UMUHIMU WA USHIRIKA KUFUNDISHWA SHULENI-DKT TIZEBA

Dkt Charles Tizeba, Waziri wa Kilimo

Na Mathias Canal-WK, Mwanza

"Mhe Waziri Mkuu Jana tulikuwa na kongamano la Kitaifa la wanaushirika Tanzania ambalo liliambatana na maonesho ya bidhaa na shughuli zinazofanywa na vyama vya ushirika kote nchini sambamba na hilo wanachama wamepata fursa ya kubadilishana uzoefu, na kujadili mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo katika uendeshaji wa sekta ya ushirika nchini, nimejiridhisha kwamba kuna umuhimu wa kuwa na somo la ushirika kwenye mitaala yetu mashuleni" 

Kauli hiyo ilitolewa juzi tarehe 7 Julai 2018 na Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba wakati akitoa salamu za Wizara ya Kilimo kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa kwenye sherehe za kilele cha siku ya ushirika Duniani.

Katika sherehe hizo zilizofanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza, Waziri Tizeba alieleza kuwa changamoto kubwa inayopelekea wananchi wengi kutotambua umuhimu wa ushirika nchini inasababishwa na kutofahamu tija ya ushirika tangu wakiwa wadogo jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya ushirika chombo ambacho ni dira na taswita ya mafanikio kwa wakulima.

Aliongeza kuwa miongoni kwa ajenda muhimu kwake kwa sasa itakuwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na Wizara ya elimu ili kuona namna bora ya kuingiza kwenye mtaala somo litakalohusu ushirika kwani kufanya hivyo wakulima watapata utambuzi juu ya umuhimu wa ushirika nchini na hatimaye kuwawezesha kiuchumi.

Alisema kuwa kumekuwa na tatizo kubwa kwa wakulima, baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika  la kukosa uzalendo na utambuzi kuhusu ushirika hivyo kudumbukia kwenye wimbi la ubadhilifu wa Mali za ushirika kwa manufaa yao pekee pasina kuwanufaisha wanachama wote.

"Kuingiza ushirika kwenye mitaala yetu mashuleni kutaibua ufahamu kwa wakulima na kuwaongezea ujuzi kama ambavyo tumekuwa na somo la stadi za kazi lililowasaidia wananchi kuwa na ujuzi wa mambo mbalimbali" Alikaririwa Dkt Tizeba

Siku ya ushirika Duniani mwaka 2018 ilipambwa na kauli mbiu isemayo "Ushirika kwa ulaji na uzalishaji endelevu wa bidhaa na huduma" ikiwa imelenga kukumbusha kwamba vyama vya ushirika sharti vihakikishe vinajitangaza na kutafuta Masoko ya bidhaa na huduma zake kwa jamii nzima.

Alisema kuwa pamoja na kwamba serikali inatambua kuwa ushirika ni nyenzo muhimu ya kuwasaidia wananchi katika upatikanaji wa mtaji na kuwawezesha kuunganisha nguvu zao za kiuchumi katika kujiendeleza kiuchumi lakini kuongezwa somo la ushirika kwenye mtaala wa elimu italeta mageuzi makubwa kwa wakulima.

Alisema kuwa pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanahamasishwa na hatimae kujiunga kwenye vyama vya ushirika kulingana na shughuli zao za kiuchumi ili kuondoa dhana  ya kudhani kwamba vyama vya ushirika ni kwa ajili ya Kilimo cha Mazao ya biashara ya nchi za nje lakini juhudi hizo zitakuwa na mabadiliko chanya zaidi kama ushirika utafundishwa mashuleni.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment