Tuesday, July 17, 2018

MHE MGUMBA AIPONGEZA (NFRA) KWA KUPATA HATI SAFI KWA MIAKA SABA MFULULIZO

Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akisisitiza ushirikiano kazini wakati akizungumza na watumishi wa wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula mara baada ya kutembelea Ofisi za wakala zilizopo Mtaa wa Relini-Kizota nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, Leo 17 Julai 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula Bi Vumilia L. Zikankuba (Wa pili kushoto) akimtembeza Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) (Wa pili kulia) ili kujionea hali ya uhifadhi wa mahindi kwenye maghala wakati akiwa katika ziara ya kikazi, Leo 17 Julai 2018. Wengine pichani ni Kaimu Meneja NFRA Kanda ya Arusha Ndg Ramadhan A. Nondo, Mkurugenzi wa maendeleo ya biashara Ndg Mikalu Mapunda na Meneja NFRA Kanda ya Dodoma Ndg Felix Ndunguru.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula Bi Vumilia L. Zikankuba akitoa taarifa ya NFRA mbele ya Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) mara baada ya kutembelea Ofisi za wakala zilizopo Mtaa wa Relini-Kizota nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, Leo 17 Julai 2018.
Picha ya pamoja kati ya Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) pamoja na timu ya Menejimenti sambamba na mameneja wa Kanda NFRA

Na Mathias Canal-NFRA, Dodoma

Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameupongeza Uongozi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kwa kupata hati safi na isiyo na mashaka kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG ) katika kipindi cha miaka saba mfululizo kuanzia 2011/2012 hadi 2017/2018.

Naibu Waziri huyo ametoa pongezi hizo leo 12 Julai 2018 wakati akizungumza na watumishi wa wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula mara baada ya kutembelea Ofisi za wakala zilizopo Mtaa wa Relini-Kizota nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma.

Alisema kuwa kupatikana kwa Hati safi isiyokuwa na mashaka kwa NFRA ni matokeo ya ushirikiano uliopo baina ya watumishi wote uliopelekea ofisi ya CAG kujiridhisha kuwa uendeshaji wa wakala ni mzuri ikiwemo udhibiti na usimamizi bora wa fedha.

“Sio jambo dogo na jepesi CAG kutoa hati safi na isiyo na mashaka kama watu wengi wanavyofikiri lakini kwa taasisi zinazofanikiwa kuingia katika heshima hiyo basi zimefanya juhudi binafsi ambazo zinahitaji kupongezwa kwa karibu nami kama kiongozi wenu sina budi kuwapongeza kwa jambo hilo zuri” Alikaririwa Mhe Mgumba na kuongeza kuwa

Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serilkali nchini CAG anazitunuku hati safi ya hesabu na matumizi sahihi ya Fedha za Umma, baada ya kufanya ukaguzi na kujiridhisha na matumizi yaliyozingatia taratibu, Sheria na kanuni za fedha  za Umma  kwa mwaka husika wa Fedha.
Naibu Waziri huyo wa kilimo nchini amewasihi watumishi hao kuendeleza juhudi za kuhakikisha wanapata hati zinazoridhisha ili kutekeleza kwa ufasaha dhamita ya NFRA ya Kuhakikisha usalama wa chakula nchini kwa kununua, kuhifadhi na kuzungusha akiba ya chakula kwa ufanisi na tija.  
Awali, akisoma taarifa ya Wakala, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Bi Vumilia L. Zikankuba pamoja na pongeza kwa waziri Mgumba kuaminiwa kwa uchapaji kazi hatimaye kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kuwa Naibu waziri wa kilimo, alisema kuwa NFRA imejipanga kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa mujibu wa sheria katika masuala ya Maendeleo huku akisema kuwa hati ni kipimo na kigezo cha kuonesha utendaji bora wa wakala.
Aliahidi kuendeleza ushirikiano bora baina ya wafanyakazi wote sambamba na ushirikiano uliotukuka na Wizara ya kilimo ili kuendeleza heshima na tija katika kuwahudumia wananchi hususani wakulima kote nchini.

Kwa mujibu wa kanuni  za ukaguzi, Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali mara baada ya kukamilisha ukaguzi wake kwa mwaka wa fedha husika, anaweza kutoa moja kati ya hati zifuatazo Hati safi, Hati yenye mashaka au Hati chafu.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment