Na
Mwandishi Maalum
Mtandao
wa Kuendeleza Vijana wenye vipaji (VPN) umekutana na wadau jijini Dar es Salaam
na kuhamasisha wadau wa mtandao huo na watu wengine kuchangia fedha kusaidia
vijana walio na vipaji lakini wazazi wao hawana uwezo kwa ajili ya kuwasomesha
katika elimu ya sekondari.
Mtandao
huo ulioanzishwa mwaka 2015 kwa lengo la kuwabaini na kufadhili vijana wenye
vipaji walio hitimu elimu ya msingi na kidato cha nne lakini familia zao hazina
uwezo wa kuwasomesha unataka kuwaendeleza vijana kimasomo ili waweze kutoa
mchango katika jamii kwa manufaa ya taifa.
Akizungumza
wakati wa hafla ya kuchangisha fedha iliyoambatana na futari kwa wadau wa
mtandao huo, mgeni rasmi ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu Gloucester & Oxford Holdings ya nchini
Uingereza Ahmed Dibibi mbali na kushauri watu kuchangia ili kusaidia vijana
walio na vipaji, ametaka vijana walio na vipaji kuangaliwa mienendo yao wakiwa majumbani ili wasiweze kupotea.
Amesema,
iwapo vijana hao hawatakuwa na uangalizi mzuri majumbani mwao basi kuna hatari
wakapotea kwa kujiingiza katika mambo yasiyofaa na hivyo kuenda kinyume na
maadili sambamba na kupoteza vipaji vyao.
Aidha,
ameshauri wazazi kuhakikisha kunakuwa na mipaka katika matumizi ya simu za
mkononi kwa vijana hasa katika mitandao ya kijamii kwani watu wengi wamekuwa
wakitumia muda mwingi katika simu badala ya shughuli za kujiletea maendeleo.
‘’sasa
hivi simu zina mambo mengi kama vile instragram na facebook tuwe na mipaka
katika matumizi ya simu, ifikie mahali tujiwekee muda wa kutumia simu ‘’
alisema Dibibi.
Kwa
mujibu wa Mtendaji huyo, kama wazazi wanataka mafanikio kwa vijana wao basi wawahimize
katika masuala ya mafanikio na kuacha kutumia muda mrefu katika kupumzika na
kusisitiza kuwa kila wakati vijana watake kujua elimu ya jumla ambayo
itawasaidia sana katika mambo mbalimbali.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Kuendeleza vijana wenye vipaji Haji Mrisho
amesema, tangu kuanzishwa kwa mtandao huo mwaka 2015, wameweza kuwasaidia
wanafunzi 151 kutoka mikoa mbalimbali.
Amesema,
mtandao wake unawatafutia wanafunzi shule bora pamoja na mfadhili binafsi
atakayekuwa tayari kugharamia gharama za masomo kwa mwanafunzi mwenye vipaji
katika shule atakayochaguliwa.
Kwa
mujibu wa Mrisho, mtandao wa VPN pia una malengo ya kuwasaidia wanafunzi wenye
vipaji katika ngazi ya chuo kikuu sambamba na kuangalia uwezekano wa kuwasaidia
wale walio na vipaji laikini hawana elimu yoyote lengo likiwa ni kuwainua na
kuendeleza vipaji vyao.
No comments:
Post a Comment