Friday, May 18, 2018

WAZIRI MKUU AKEMEA UHARIBIFU WA MIUNDOMBINU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea uharibifu wa makusudi wa miundombinu ya barabara na majengo unaofanywa na baadhi ya wananchi na kuwataka waache tabia hiyo mara moja.

Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Mei 17, 2018) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Magu, Bw. Kiswaga Destery aliyetaka kujua Serikali inachukua hatua gani dhidi ya wananchi wanaoharibu miundombinu ili wakauze kama vyuma chakavu kwa vile Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu hiyo.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatumia fedha nyingi sana kuboresha miundombinu mbalimbali nchini na kwamba kila Mtanzania anao wajibu wa kulinda miundombinu hiyo.

“Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu ya barabara na majengo ili kutolea huduma, Watanzania wote tunao wajibu wa kuilinda na endapo itatokea mtu anaihujumu miundombinu hii, Serikali hatuwezi kukaa kimya, lazima tutachukua hatua,” ameonya.

Amesema jukumu la ulinzi ni la Watanzania wote, na kila Mtanzania anayo dhamana ya ulinzi na usalama wa ndani ya nchi ikiwemo kuilinda miundombinu. “Juzi niliona kwenye televisheni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mheshimiwa Jaffo akishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Shinyanga, wamekamata Fuso lililojazwa vyuma vilivyong’olewa kwenye barabara, ni vile ambavyo vinawekwa kwenye daraja na kingo za barabara,” amesema.

“Huu ni uharibifu ambao hatuwezi kuvumilia, na katika hili Watanzania lazima tuungane pamoja tukemee tabia hii. Tunatumia fedha nyingi kujenga kingo za barabara, kuashiria maeneo yenye hatari lakini Watanzania wengine wanakuja kung’oa kwa matumizi yao. Mimi naamini Mkoa wa Shinyanga utakuwa umechukua hatua kali dhidi yao,” amesema.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, MEI 17, 2018.

No comments:

Post a Comment