Wednesday, May 30, 2018

MASHINDANO YA UMISETA KUANZA WIKI IJAYO JIJINI MWANZA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo akipiga mpira kuashiria ufunguzi wa matangazo mubashara ya mashindano ya UMITASHUMTA  na UMISETA yatakayofanyika jiji Mwanza

 Kikundi cha ngoma 
 Wanafunzi wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo 
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo  akizungumza katika ufunguzi wa matangazo mubashara ya mashindano ya UMITASHUMTA  na UMISETA yatakayofanyika jiji Mwanza

Wanafunzi wa shule wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Joyce Ndalichako akicheza mpira wa pete na mmoja wa wanafunzi.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk.Harrison Mwakyembe akimrushia mpira Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo


.....................................................
Mashindano ya michezo ya Umoja wa Michezo wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA) yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 4 juni, 2018 jijini Mwanza.

Mashindano ya michezo ya UMISSETA ngazi ya Taifa yataanza tarehe 04 juni 2018 hadi tarehe 15 juni 2018 katika viwanja vya chuo cha ualimu cha butimba jijini Mwanza na kufuatiwa na mashindano ya UMITASHUMTA ambayo yatafanyika katika viwanja hivyo hivyo kuanzia tarehe 17 juni 2018 hadi tarehe 29 juni 2018.

Mashindano hayo ya UMISSETA na UMITASHUMTA yanatarajiwa kuonyeshwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha AZAM kutoka jijini Dar es salaam

Akizungumza kwenye ufunguzi wa matangazo ya moja kwa moja ya Televisheni ya AZAM uliofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo alikipongeza kituo cha AZAM TV kwa kukubali kuyatangaza mashindano hayo ambayo ndiyo chimbuko la michezo nchini.

Waziri Jafo alisema kuwa kwa namna ya pekee mwaka huu mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA yataonyeshwa moja kwa moja na kwenye Televisheni na hivyo kuwawezesha watanzania kujionea vipaji mbalimbali vya watoto wao.

Pia Waziri Jafo aliwaagiza Maafisa Elimu wa Mikoa hasa wanaosimamia michezo nchini kuhakikisha wanawapeleka walimu wa michezo waliofundishwa katika shule za michezo ili wafundishe shule maalum zilizotengwa kuandaa vijana kimichezo.

“Waziri Ndalichako unasimamia sera na umetoa maelekezo kwa mujibu wa sera na hivi sasa kila mkoa tuna shule zipatazo mbili za michezo,na bahati nzuri kwa taarifa za wataalam wangu shule zile zimeanza kusimamiwa vizuri kwa kuinua vipaji vya vijana wetu ndani ya nchi yetu,naomba mlisimamie,”alisisitiza waziri Jafo.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Profesa Joyce Ndalichako pamoja na kupongeza hatua hiyo ya AZAM TV pia aliagiza Mikoa kuhakikisha kuwa inatekeleza agizo la kutenga shule mbili maalum kwa ajili ya michezo na kuhakikisha kuwa mamlaka husika zinapeleka walimu waliosomea fani ya michezo

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe aliipongeza hatua hiyo ya AZAM Televisheni kwani kuonekana kwa mashindano hayo kutachochea ari ya vijana wengi nchini kupenda michezo.

Mapema Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bwana Tixon Nzunda alisema kuwa katika mashindano ya mwaka huu jumla ya wanamichezo 3,360 kutoka mikoa 28 ikiwemo miwili kutoka Zanzibar watashiriki kwenye UMISSETA  ambapo michezo 10 itashindanishwa.

Bwana Nzunda aliongeza kuwa kwa upande wa UMITASHUMTA jumla ya wanamichezo 3120 kutoka mikoa 26 ya Tanzania bara watashiriki ikiwa ni wachezaji 120 kila mkoa.

Jumla ya michezo 9 ikiwemo mpira wa miguu wavulana na wasichana, mpira wa miguu maalum (wavulana viziwi), Netibali kwa wasichana, mpira wa wavu, mikono, kengele kwa wasioona, riadha maalum, riadha kawaida na sanaa za maonyesho.

No comments:

Post a Comment