Judith Ferdinand, Mwanza
Ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora, jitihada za dhati zinahitajika kutoka kwa wadau, jamii pamoja na serikali.
Pamoja na juhudi zilizopo, bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa matundu ya vyoo, madarasa, makazi na ofisi za walimu pamoja na nyenzo za kufundishia.
Ikiwa miundombinu ya elimu itaboreshwa, Taifa litazalisha vijana bora na wenye maarifa kwani watasoma katika mazingira salama na kwa bidii.
Akizungumza ijumaa Disemba 15 mwaka huu katika kikao na wanahabari Jijini Mwanza cha kutambuana na kufanya kazi pamoja, Afisa Miradi kutoka Mtandao wa Elimu Tanzania TenMet, Moses Gwerino alisema sekta ya elimu nchini inakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo hazipimwi kwa eneo moja bali zinagusa maeneo mengi nchini.
Gwerino alisema ukosefu wa elimu bora husababisha changamoto ya ukosefu wa ajira wananchi wengi hushindwa kujiajiri na kubuni kutokana na kukosa weledi.
Aisha alisema kuwekuwa na changamoto ya udanganyifu kwenye mitihani kwa baadhi ya shule nchini ili zioneka zinafanya vizuri kimasomo, jambo ambalo huchangia kudumaza sekta ya elimu na pia kuwapotosha wahitimu.
Katika hatua nyingine alisema sekta ya elimu nchini inaweza kuboreshwa ikiwa kamati za usimamizi wa shule zitaimarishwa ili kuwa sehemu ya kusimamia na kufuatilia matumizi ya ruzuku, pembejeo na rasilimali kwenye ngazi ya jumuiya za shule.
Naye Afisa Habari, Mawasiliano na Tehama kutoka TenMet, Dominic Dogani alisema lengo la kukutana na waandishi wa habari ni kuweza kushirikiana pamoja katika kutatua changamoto zinayoikabili sekta ya elimu kwa kufikisha ujumbe kwa viongozi na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Naye mwanahabari Sheila Katikula alisema kuna haja kwa serikali, wadau na jamii kushirikiana ili kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa kutatua changamoto zilizopo mijini na vijijini kwani zote zinafanana.
No comments:
Post a Comment