Wednesday, December 20, 2017

JAFO AAGIZA MANISPAA DODOMA IPIME HARAKA VIWANJA NA AMFAGILIA MBUNGE MAVUNDE KWA KUWAJALI WANANCHI






Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Selemani Jafo amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma  Godwin Kunambi kuhakikisha wanapima viwanja haraka ili kuufanya mji wa Dodoma uendane na kasi ya ongezeko la idadi ya watu wanaohamia Dodoma na kuufanya mji uliopangwa kwa utaratibu unaoeleweka.

Jafo ameyasema hayo leo katika hafla fupi ya kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Shule ya Sekondari Iyumbu-Dodoma Mjini,ambapo pia ametumia nafasi hiyo kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wake na kuahidi kuendelea kumpa ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wake wa Jimbo la Dodoma Mjini.

Mbali na hilo, Jafo ameagiza fedha kiasi cha  sh.milioni 10 zilizopo kwenye akaunti ya kata hiyo ambazo zilitakiwa kutumika kupaulia darasa la shule ya sekondari Iyumbu  kutumika kujenga madarasa manne.

Kwa upande wake, Mavunde amesema katika Manispaa ya Dodoma kuna upungufu wa vyumba vya kusomea zaidi ya 1000.

Amesema wamekubalina na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuanzisha kampeni maalumu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kupitia wadau mbalimbali ambapo wao watapokea vifaa tu kama Saruji.

Awali katika hafla hiyo,Mkurugenzi wa Manispaa  Kunambi amesema tayari Manispaa imeshatoa Sh.Milioni  10 kusaidia ujenzi huo na pia ameahidi kusimamia ujenzi wa Sekondari hiyo ili kuwaondolea adha wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule za Sekondari.

Wakizungumzia hatua hiyo, Wananchi wa kata Iyumbu wameshukuru sana jitahada za viongozi katika kuwaletea maendeleo na kutatua changamoto zao na kuahidi kujitolea kukamilisha ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment