Tuesday, November 28, 2017

WAZIRI MKUU APOKEA VIFAA VYA MASHINDANO YA MAJIMBO



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. milioni 50 kwa ajili ya kuanzisha mashindano ya mpira wa miguu kwa majimbo ya mkoa wa Dar es Salaam.

Vifaa hivyo vimetolewa na Muwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza na Muwakilishi wa kuteuliwa Bw.Ahmada Yahya Abdulwakili, ambapo mara baada ya kupokea vifaa hivyo alivikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda.

Amepokea vifaa hivyo jijini Dar es Salaam leo (Jumanne, Novemba 28, 2017), mashindano hayo yatakayoratibiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) yatahusisha vijana kutoka majimbo yote 10 ya mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amewapongeza Bw. Raza na Bw. Ahmada kwa kuona umuhimu wa vijana kushiriki katika michezo na kuamua kudhamini mashindano hayo, ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya gari aina ya Carry lenye thamani ya sh. milioni saba.

Amesema mashindano hayo yatawawezesha vijana kupata fursa ya kuonyesha na kukuza vipaji vyao na kusisitiza kwamba michezo ni muhimu kwani ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 na pia inakuza ajira, hivyo ameagiza mashindano hayo yasimamiwe kikamilifu kwa kufuata sheria za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Bw. Raza amesema sababu ya kudhamini mashindano hayo upande wa Zanzibar na Tanzania Bara ni kumuunga mkono Rais Dkt John Magufuli katika utekelezaji wa ilani.

Amesema mashindano kama hayo yalifanyika kwa mafanikio makubwa Zanzibar ambapo Raza na wanaCCM wenzake waliyadhamini. Hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara kudhamini mashindano kama hayo ili kuwawezesha vijana kukuza vipaji vyao.

Kwa upande wake Bw. Makonda alimuahakikishia Waziri Mkuu kwamba watayasimamia kikamilifu mashindayo kwa sababu ni chachu ya kukuza vipaji vya mpira wa miguu mkoani Dar es Salaam.

Pia alimueleza Waziri Mkuu dhamira ya mkoa huo ya kuanzisha kituo cha muziki “Music hub” ili kuwawezesha vijana wenye vipaji vya muziki jijini Dar es salaam, kupata fursa ya kuendeleza  vipaji vyao.

Mashindano ya majimbo Zanzibar yalizinduliwa Machi 23, 2017 na Rais wa Zanzibar Dkt. Mohammed Shein na kufungwa Novemba 25, 2017 na Waziri Mkuu, ambapo mshindi wa kwanza alipewa zawadi ya gari aina ya Carry lenye thamani ya shilingi  milioni saba.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, NOVEMBA 28, 2017.

No comments:

Post a Comment