Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo ametoa wito kwa wafanyabiashara wote nchini ambao wanahitaji
mahindi kufika haraka katika mkoa wa Rukwa kununua zao hilo kwani
kumekuwa na ziada ambayo wananchi wanahitaji kuuza lakini soko hakuna.
Amesema kuwa katika wilaya ya
Nkasi pekee kuna zaidi ya tani 23,000 za chakula ambacho ni ziada ya
wilaya na imekosa wanunuzi na kumuagiza katibu tawala wa Mkoa
kuhakikisha anafanya mawasiliano na mikoa mingine ambayo ina upungufu wa
chakula ili kuja kununua ziada hiyo ambayo wananchi wamekuwa
wakilalamika kukosa soko.
Pia, amemuagiza katibu tawala wa
Mkoa kuhakikisha kuwa kunakuwa na mratibu wa mahindi katika kila wilaya
ili kuwasaidia wafanyabiashara wa mahindi kutoka nje ya mkoa kupata
urahisi wa kununua mahindi na kuwaepusha na utapeli.
“Tani zaidi ya 23,000 ipo kwenye
wilaya moja tu, hii ni fursa kwa wafanyabiashara waliopo kwenye mikoa
ambayo ina upungufu wa chakula kuja kununua mahindi na kuyapeleka huko
wankoyahitaji, hivyo nakuagiza katibu tawala kuhakikisha kuwa unafanya
mawasiliano na mikoa na ambayo ina upungufu pamoja na wafanyabishara
wenye kuhitaji ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu lakini kuwe na
mratibu wa kuweza kusimamia hili ili wafanyabiashara hao wasipate tabu,”
Ameyasema hayo baada ya kusomewa
taarifa ya wilaya ya Nkasi iliyobainisha uwepo wa ziada ya tani 23,000
za mahindi kwaajili ya kuuza ambapo wakulima wa wilaya hiyo na
kwengineko Mkoani humo wamekuwa wakilalamikia soko la zao hilo.
Kwa upande wake Kaimu Katibu
Tawala wa wilaya ya Nkasi Mwanaisha Luhaga alipokuwa akisoma taarifa
hiyo alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili hivi sasa ni
upatikanaji wa mbolea kwa wananchi ambapo mpaka sasa wilaya imepokea
tani 20 tu kati ya 850.
No comments:
Post a Comment