Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.
Binilith Mahenge na ujumbe alioambatana nao wakikagua mradi wa maji ya
chemichemi kwenye kijiji cha Kongwa Maji
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.
Binilith Mahenge na ujumbe alioambatana nao wakikagua mashine ya
kusukumia maji kwenye mradi wa maji ya chemichemi kijijini Kongwa Maji
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge akihutubia mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Suguta Wilayani Kongwa.
Mkuu wa Mkoa Dodoma Dkt. Binilith
Mahenge akiwasalimia Watoto wenye Ulemavu wa Viungo na matatizo ya
akili wanaotibiwa kwenye kituo cha Watoto cha Mlali Kongwa.
……………………………………………………………………….
Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk.
Binilith Mahenge amesema Mkoa wa Dodoma hauna sababu zozote za kukumbwa
na tatizo la upungufu wa Chakula wala Njaa kwa wananchi wake kwa kuwa
unazo fursa za kutosha za kuzalisha mazao ya chakula yanayotosheleza
mahitaji ya Mkoa.
Aidha amesema mkoa huo una fursa za kuzalisha mazao ya biashara yatakayoweza kuwainua kiuchumi wa mwananchi na Mkoa kwa ujumla.
Dk. Mahenge ameyasema hayo
mwishoni mwa wiki akiwa katika ziara Wilayani Kongwa ikiwa ni mwendelezo
wa ziara yake ya kutembelea Wilaya za Mkoa wa Dodoma.
Kufuatia hali hiyo, Mkuu huyo
amewataka Viongozi na wataalamu kuwasimamia wananchi kupanda mazao
yanayotumia maji kidogo na kustawi kwa ufanisi Mkoani Dodoma kama Mtama,
Uwele, Muhogo, Alizeti na Sasa zao la Korosho lililothibitika kustawi
vizuri kwenye Ardhi ya Dodoma.
Aidha amewataka viongozi na
Wataalamu wa kilimo wa Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma kuhakikisha
wanawaelimisha na kuwasimamia wananchi kutekeleza mkakati wa kilimo wa
Mkoa unaolenga kuzalisha chakula cha kutosheleza mahitaji ya Mkoa, kwa
kuachana na kilimo cha mazoea badala yake unasisitiza kilimo cha
maarifa, na cha kisasa.
Amewatoa hofu wananchi kuwa zao
la mtama mbali na kutumika kama chakula lakini lina soko la uhakika kwa
ajili ya viwanda vya kutengeneza vinywaji hivyo hata kama mwananchi
hataki kula mtama anaweza kuuza na akanunua chakula anachokitaka
mwenyewe lengo likiwa kuwa na uhakika wa chakula.
Amempongeza Mkuu wa Wilaya ya
Kongwa Deogratias Ndejembi kwa kuanzisha kampeni ya kuondoa njaa
wilayani Kongwa (ONJAKO) na kuzitaka Wilaya nyingine kuiga mfano huo.
Awali, akielezea Kampeni ya
ONJAKO Mkuu huyo wa Wilaya amesema kwenye wilaya hiyo kila kaya, pamoja
na mazao mengine ni lazima kulima heka mbili (2) za mtama kwa ajili ya
chakula na endapo kaya yoyote itakayokaidi muhusika atalazimika kulipa
faini isiyopungua shilingi elfu hamsini (50) na endapo atashindwa basi
adhabu ya kifungo cha miezi mitatu (3) itamkabili, Lengo likiwa
kuhakikisha kila kaya inazalisha chakula cha kutosheleza mahitaji
yake.
Kadhalika, Dk.Mahenge amemuagiza
Katibu Tawala wa Mkoa Rehema Madenge kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa
Halmashauri za Wilaya Mkoani Dodoma kuhakikisha kila Wilaya ina ainisha
mahitaji ya vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya elimu ili vifaa hivyo
vinunuliwe kwa mfumo wa pamoja moja kwa moja kutoka Viwandani baada ya
kupata idhini ya Wizara ya Kisekta lengo likiwa kupunguza gharama za
vifaa.
Amepiga marufuku tabia za
viongozi na Wakuu wa Idara kwenye Wilaya kukaa tu ofisini na kuwataka
waweke ratiba ya mara kwa mara ya kutembelea shule kufanya ukaguzi ili
kubaini changamoto halisi zinazo kabili hali ya utoaji elimu na
kuzitafutia majibu ya kudumu, pia ametaka Wilaya ziwape walimu
ushirikiano unaohitajika ili waweze kutekeleza jukumu la kuwafundisha
watoto kwa ufanisi zaidi.
No comments:
Post a Comment