Thursday, November 9, 2017

Rais Magufuli atembelea shamba la miwa na kiwanda cha sukari cha Kagera

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 08 Novemba, 2017 ametembelea shamba la miwa na kiwanda cha sukari cha Kagera (Kagera Sugar) kilichopo Wilayani Misenyi na kuagiza viwanda vyote vya kuzalisha sukari nchini kutafuta namna ya kuongeza uzalishaji ili kumaliza tatizo la upungufu wa tani 130,000 unaoikabili nchi kwa sasa.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kutembelea shamba la miwa linalolimwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya umwagiliaji (Centre Pivot) na kiwanda cha sukari cha Kagera ambacho uzalishaji wake kwa sasa ni tani 75,000 za sukari kwa mwaka ambazo zinaungana na tani nyingine 245,000 kutoka viwanda vingine nchini kufanya uzalishaji wa jumla ya tani 320,000 kiwango ambacho ni pungufu ikilinganishwa na mahitaji ya tani 420,000.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Seif Seif amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa hatua alizochukua kudhibiti uingizaji wa sukari hapa nchini na kueleza kuwa kabla ya kuchukua hatua hizo wazalishaji wa sukari walishaamua kufunga viwanda vyao kutokana na kukithiri kwa uingizaji holela wa sukari kutoka nchi za nje tena bila kuzingatia ubora na usalama kwa walaji.

Bw. Seif amebainisha kuwa hatua zilizochukuliwa na Mhe. Rais Magufuli zimewasaidia wazalishaji wa sukari kuanza kupiga hatua katika uwekezaji ambapo shamba la Kagera linalolima hekta 14,000 kwa mwaka na kuzalisha tani 75,000 za sukari limepanga kuendelea kupanua mashamba yake hadi kufikia hekta 30,000 na uzalishaji wa tani 170,000 za sukari ifikapo mwaka 2022.

Pamoja na kuipongeza Kagera Sugar kwa kufufua kiwanda hicho kilichokufa baada ya kupigwa mabomu wakati wa vita vya Kagera, Mhe. Rais Magufuli ambaye amezungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho, amekubali ombi la kujengwa kwa daraja katika mto Kagera litakalounganisha shamba hilo na Wilaya ya Karagwe ambako upanuzi wa kilimo cha miwa umepangwa kufanywa, na pia ametoa wito kwa mwekezaji huyo kuitumia benki ya kilimo (TAB) kupata mikopo.

“Shamba na kiwanda hiki mnaajiri watu 5,000 nawapongeza sana na sisi Serikali ni lazima tuwaunge mkono, kuhusu ombi la daraja, tutalijenga na nakuagiza Katibu Mkuu wa Ujenzi Bw. Joseph Nyamuhanga ifikapo Januari 2018 muanze kujenga, kwa kuwa Bw. Seif ameshanunua vyuma vya ujenzi, na pia tumepata fedha kutoka benki ya maendeleo Afrika (AfDB) Shilingi Bilioni 242, hizo zote tunazipeleka kwenye benki ya kilimo, Bw. Seif sasa nenda ukakope huko, na ukikopa uelekeze kwenye kilimo” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali pendekezo la kuwatumia wazalishaji wa sukari wa hapa nchini kuagiza sukari inayopungua ili kukidhi mahitaji ya nchi, lakini ameonya kuwa mwanya huo usitumiwe kuingiza sukari isiyo bora na salama na ametaka utaratibu huo ufanywe kwa muda mfupi wakati viwanda vinaongeza uzalishaji wake ili hatimaye Serikali ipige marufuku uingizaji wa sukari kutoka nje ya nchi.

Pia, amempa siku tatu Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba kuwaondoa mara moja Maafisa wote waliokuwa wakitoa vibali kwa waingizaji wa sukari hapa nchini kutokana na vitendo vyao vya kutoa vibali hovyo na hivyo kudhohofisha viwanda vya ndani.

Kabla ya kufika Kagera Sugar Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Bunazi na kusikiliza kero zao ikiwemo ya kuuziwa sukari kwa bei ya juu ikilinganishwa na bei ya Bukoba Mjini, na kufuatia kero hiyo ameitaka Kagera Sugar kumpa uwakala mfanyabiashara wa Bunazi Richard Lulinda ili aweze kuwauzia sukari wananchi wanaozunguka shamba hilo kwa bei nafuu.

Kuhusu kero ya wananchi wa Bunazi kukodishwa mashamba ya kulima mazao katika eneo la kijiji Mhe. Rais Magufuli amepiga marufuku ukodishaji huo na amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya kukamilisha majengo ya shule ambayo viongozi wa kijiji walidai wanakamilisha ujenzi huo kwa kutumia fedha za kukodisha maeneo ya kijiji.

Akiwa anarejea Bukoba Mjini Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Rwamishenye na kupokea kero zao ambapo pamoja na kuwachangia Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya shule amewataka wawaambie viongozi wao kata na mitaa kufikisha Serikalini andiko la kujengewa Soko.

Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Bukoba

08 Novemba, 2017

No comments:

Post a Comment