Tuesday, November 7, 2017

MWIGULU AFUNGUA KAMPENI ZA UDIWANI KATA YA SIUYU-IKUNGI

Na Mathias Canal, Singida

Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) jana Novemba 7, 2017 amezindua kampeni za Udiwani Kata ya Siuyu Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida huku akisindikizwa na viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi CCM akiwemo Mwenyekiti wa Chama na katibu wa CCM Mkoa wa Singida.

Katika mkutano huo wa kampeni uliohudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wananchi wamejitokeza kwa wingi huku wakiuga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Tano tangu kuingia madarakani katika kipindi cha miaka miwili hivi sasa.

Akizungumza katika mkutano huo wa uzinduzi wa kampeni Mhe Mwigulu alisema kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya awamu ya tano kumekuwa na matokeo chanya jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaiimarisha nchi katika ufanisi kiweledi ikiwa ni pamoja na kukua kwa uchumi wan chi na mtu mmoja mmoja.

Alisema kuwa kuzuia CCM kushinda ni kama vile kuzuia maji kupita katika mkondo wake jambo ambalo haliwezekani hivyo kuwaomba ridhaa wananchi wote kumchagua mgombea wa CCM katika nafasi ya udiwani ili akawasilishe hoja zao tofauti na vyama vingine ambavyo kazi yao ni kupinga.

" Tochi haiwezi kuwaka endapo kama utachanganya Betri na gunzi, hivyo kuchagua Rais wa CCM, huku nafasi zingine zinaenda kwa upinzani ni kuchanganya gunzi na Betri katika Tochi hivyo haiwezi kutoa mwanga hata wa kuibia tu”

“Kuchagua vyama vya upinzani ni kuruhu maendeleo kupingwa kwani tangu kuanzishwa kwa vyama vingi, vyama vya upinzani havijawahi kupongeza juhudi za serikali wala havijawahi kukubali tunachokifanya vyenyewe siku zote huwa ni kupinga tu” Alisema Mwigulu

Aliongeza kuwa Ushindi wa CCM Kata ya Siuyu utanakshiwa na amani, Haki, Usawa na Demokrasia kama ilivyo Desturi ya CCM inapoingia katika uchaguzi huku akiwaomba wananchi kumchagua Mgonto Ramadhan Juma ambaye ni mgombea wa CCM mwenye sifa za kuwa kiongozi.

Aidha, Alisema katika uchaguzi mdogo haichaguliwi sera mpya kwani ilani ya CCM ilishapewa ridhaa ya kushika dola hivyo mgombea wa CCM pekee ndiye mbeba maono kwani ilani anaifahamu ilani ya ushindi ambayo ndio mkataba halisia kati ya wananchi na chama cha mapinduzi.

Mhe Mwigulu aliwasihi wananchi kwa kauli moja kutochagua wagombea wa upinzani kwani vyama vyao  vimevamiwa na viongozi wasaka  madaraka huku wakikosa sifa ya kupigania  maendeleo na kukosa ujasiri wa kutetea maslahi ya umma.

Mwigulu alisema kuwa kumchagua diwani wa CCM ni dalili nzuri ya kumpongeza na kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu alionya vyama vya siasa kutumia vibaya majukwaa ya siasa kuitukana serikali na viongozi wote badala ya kuzungumzia ajenda ya maendeleo kwani wananchi wamechoshwa na porojo za kisiasa za visa na mikasa bali wanataka maendeleo.

Mhe Mtaturu alisema kuwa Serikali ya CCM itahakikisha inaendelea kuboresha zaidi mazingira ya kufundishia ambapo tayari wameanzisha mfuko wa Elimu Ikungi kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maabara, nyumba za walimu, zana za kufundishia sambamba na madarasa.

Alisema kuwa kila mwananchi anapaswa kuunga mkono juhudi hizo za serikali kwani maendeleo ni ya kila mwananchi kushiriki kwa manufaa ya watanzania wote.

Mhe Mtaturu Aliongeza kuwa ataendelea kusimamia na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika kipindi chote kuanzia mwanzo wa kampeni mpaka pale uchaguzi utakapomalizika.

Aliongeza kuwa CCM ilimkabidhi Ilani ya kuisimamia katika kipindi cha mwaka 2015-2020 hivyo Diwani wa CCM pekee ndiye mwenye uwezo na nia ya dhati atakayeendana na ilani hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa pamoja.

Katika kinyang’anyiro hicho cha udiwani katika Kata ya Siuyu Vyama vinavyowania katika kiti cha udiwani ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), CHADEMA na CUF.

MWISHO

No comments:

Post a Comment