Na Mwandishi MOHA
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amempa maelekezo Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo kuunda Kamati ya kuchunguza uvamizi wa viwanja vya Gereza Isanga
uliofanywa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) mjini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya
kumaliza ziara yake ya kikazi katika Gereza hilo, Masauni alisema eneo
hilo ambalo lina ukubwa wa ekari zaidi ya 150 lazima lirudishwe katika
himaya ya Jeshi la Magereza kama lilivyokua awali.
“Eneo hili linalimilikiwa na
Jeshi la Magereza tangu mwaka 1946, haiwezekani watu watokee na kuchukua
ardhi hii kiholelaholela, hii haiwezekani hata kidogo, lazima uchunguzi
ufanyike haraka iwezekanavyo na eneo lote lilrudi mikononi mwa jeshi,”
alisema Masauni na kufafanua;
“Serikali ilishahamia hapa mjini
Dodoma, hivyo shughuli za magereza zitaongezeka kwa kasi, na umuhimu wa
maeneo utakua mkubwa zaidi kutokana na umuhimu wa jeshi hili katika
kukuza uchumi.”
Aliongeza kuwa, jeshi hilo
linahitaji kujenga nyumba za askari kwa kasi na kutokana na changamoto
hiyo ya uvamizi uliofanywa ujenzi waweza kusuasua hivyo eneo hilo
lahitajika kurudishwa haraka sana.
Masauni alifafanua kuwa, tayari
amemuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali, Projest
Rwegasira kulichunguza suala hilo kwa kina kwa kuwa kuna taarifa ambazo
bado hazijathibitishwa kuwa kati ya wamiliki wa viwanja hivyo walikua ni
viongozi waandamizi wa CDA, Jeshi la Magereza pamoja na viongozi
wakubwa mbalimbali.
Hata hivyo, Masauni alipiga marufuku mtu yeyote kuendeleza ujenzi wa eneo hilo hata kama ana vibali vyote vya kumiliki eneo.
Aidha, Mkuu wa Gereza Isanga,
Keneth Mwambeje, akizungumzia suala hilo, alisema jeshi lake lina
nyaraka za mawasiliano kati ya viongozi wa gereza hilo ambao walikua
kwa wakati huo pamoja na waCDA.
CDA ambayo ilivunjwa na Rais John
Magufuli, ndio inahusika kugawa viwanja hivyo kwa wananchi zaidi ya mia
moja ambao baadhi yao wamejenga na wengine wanaendelea na ujenzi katika
eneo.
No comments:
Post a Comment