KILIO cha
ukosefu wa soko la nyanya linalowakabili wakulima wa mji mdogo wa Ilula na
maeneo yanayozunguka wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kimeanza kupata ufumbuzi
baada ya kiwanda cha Dabaga Vegetable kutangaza kununua tani 10 hadi 20 za zao
hilo kwa siku.
Kiwanda
hicho ambacho awali kilikuwa mjini Iringa, kimejengwa upya na kuanza uzalishaji
hivikaribuni katika kijiji cha Ikokoto kata ya Ilula wilayani Kilolo, kikiwa kimetanuliwa ukubwa wake.
Mtaalamu
wa ubora wa bidhaa za kiwanda cha Dabaga, Zainabu Miraji alisema uwezo wa
kiwanda ni kuzalisha tani 40 za nyanya kwa siku, lakini kimeanza kununua kati
ya tani 10 na 20 tu kwa siku kwa kuzingatia mahitaji ya masoko yao kwasasa.
“Nyanya
tunayohitaji ni ile yenye ubora wa daraja B iwe imekomaa ikiwa shambani,
nyekundu iliyoiva, isiwe na madoa meusi, isiwe na fangasi na wala imetobolewa
na wadudu,” alisema.
Akizungumza
na baadhi ya wakulima wa nyanya wa kata hiyo waliokuwa wakishiriki siku ya
wakulima kiwandani hapo jana, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdallah
aliipongeza kampuni mama ya kiwanda hicho ya Chai Bora akisema uamuzi wao wa
kujenga kiwanda hicho karibu na wakulima ni utekelezaji wa azma ya Rais Dk John
Magufuli ya kuifanya nchi kuwa ya viwanda.
“Wilaya
ya Kilolo ni moja ya wilaya chache zinazozalisha nyanya kwa kiwango kikubwa
nchini. Kiwanda hiki kitasaidia kwa kiwango fulani kupunguza upotevu wa nyanya
zilizokuwa zikioza kwasababu ya ukosefu wa soko,” alisema.
Ili
kiwanda hicho kizalishe kwa kiwango chake na kifikirie kupanua uzalishaji wake,
Abdallah alisema wakulima na wananchi wa wilaya hiyo wanawajibu wa kusaidia
kutangaza bidhaa zake ili zipate masoko mengi zaidi.
Aliwataka
wakulima wa mazao yanayohitajika kiwandani hapo kuzalisha kwa kuzingatia ushauri
na utaalamu unaotakiwa ili wapate bidhaa zitakazopata soko la uhakika.
Mmoja wa
wakulima wa nyanya katika kata hiyo, Yohanes Mhanda alikiomba kiwanda hicho
kizalishe kwa kiwango chake ili wakulima wauze zaidi na akasema wanao uwezo wa
kuboresha kilimo hicho kwa kuzingatia vigezo vilivyotolewa.
Akizungumzia
uzalishaji wa nyanya katika wilaya hiyo, Afisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo
wa Ilula, Edward Mbembe alisema wilaya inazalisha tani 55,000 hadi 70,000 za
nyanya kwa misimu miwili kila mwaka.
“Msimu
wa kwanza ni wa kati ya Novemba hadi Desemba na msimu wa pili ni wa kati ya
Machi hadi Juni. Kwa ujumla tuna siku 180 za uzalishaji kila mwaka,” alisema.
Alisema
kama uwezo wa kiwanda utakuwa ni kununua tani 10 kwa siku, basi kwa siku 180
kitanunua tani 1,800 na kama ni tani 20 basi kwa siku hizo kitanunua tani 3,600.
No comments:
Post a Comment