Saturday, November 25, 2017

Acacia North Mara watinga Tume ya Usuluhishi na Uamuzi CMA


Jengo la Tume ya Usuluhishi na Uamuzi CMA Shinyanga
Na Oscar Mihayo, Shinyanga
Mgodi wa Acacia North Mara umefungua kesi katika  Tume ya Usuluhushi na Uamuzi (CMA) Mkoa wa Shinyanga dhidi ya Chama cha Wafanyakazi wa Migodini Numet Tawi la North Mara kwa tuhuma za kukwamisha juhudi za ubinafsishaji wa kitengo cha ulinzi.
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa mgodi huo kutaka kubinafsisha kitengo cha ulinzi kwenye kampuni binafsi ya ulinzi migodini G4S, huku kukiwa  na sintofahamu juu ya hatima ya wafanyakazi 136 ambao ni waajiriwa na Acacia.
Shauri hilo namba 201 la mwaka 2017 limeanza kusikilizwa juzi chini ya usuluhishi wa Kilian Nembuka ambaye amesikiliza shahidi wawili upande wa mleta maombi huku shahidi mmoja wa wajibu maombi akipata udhuru na kupelekea kesi hiyo kuairishwa hadi disemba 11 mwaka huu.
Akiongea baada ya kuairishwa kesi hiyo, wakili wa mleta maombi Galati Katambi alisema wameamua kufika hatua hiyo kufuatia upande wa wafanyakazi kukwamisha mchakato wa ubinafsishaji hali iliyopelekeaa kukimbilia kwenye hatua ya usuluhishi.
“North Mara imefikia hatua ya kubinafsisha kitengo cha ulinzi na kimsingi hatua hiyo itawagharimu baadhi ya wafanyakazi kwa kuachishwa kazi na kimsingi kisheria lazima muingie makubaliano kati ya kampuni na waajiri ambapo wenzetu hawakuwa tayari na ndo tukachua hatua hii ya usuluhishi,” alisema Gallat.
Kwa upande wake wakili wa kujitegemea upande wa mjibu maombi, Ambrosi Malamsha alisema wateja wake walikuwa tayari kuendelea na mchakato wa kubinafsisha kitengo hicho lakini kuna taratibu zilikiukwa hali iliyopelekea kuona mchakato huo ni batiri.
“Kitendo cha mwajiri kuleta Voluntary Separation Package (USP) eneo la kazi na kuruhusu kufanya kazi wakati mchakato haujakamilika ilikuwa ni ishara kwamba tayari mchakato huo ni batiri na haukubaliki,” alisema Malamsha.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Tamico alisema mgodi ulipoanza hatua ya kuondoa kitengo hicho uliwashirikisha kwa kutoa mapendekezo ambayo yalikuwa yanawataka Acacia kuwafutia waajiriwa mikopo benki, nyumba na Saccos hatua ambayo haijatekelezeka.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Numet, Idd Hussein alisema kama wanataka mchakato huo uendelee ni bora ukafutwa na kuanza upya ili kuleta usawa kwa pande zote mbili.
Idd Hussein, Makamu Mwenyekiti NUMET.

No comments:

Post a Comment